Chama cha Mapinduzi CCM mkoa wa Katavi kimefanya kongamano la kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuondoa zuio la mikutano ya hadhara.
Kongamano hilo, limefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mpanda likitanguliwa na maandamano yaliyobeba ujumbe wa pongezi kwa Rais Samia kwa hatua yake ya kuruhusu Demokrasia kwa vyama vyote vya siasa nchini.
Akizungumza katika kongamano hilo Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Katavi, Idd Kimanta amesema hatua hiyo ni busara ya Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa kuruhusu mikutano ya siasa kufanyika bila zuio.
Amesema, Viongozi na wanachama wa CCM Mkoani humo wanatakiwa kujiandaa kujibu hoja za vyama vya upinzani iwapo zitaibuliwa kwa njia ya amani na kuendelea kuyasema mema yaliyofanywa na serikali.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko ametoa rai kwa vyama vya siasa kutumia fursa hiyo kunadi sera zao na kufanya siasa za kiungwana badala ya kutoa lugha za kejeli majukwaaani.
Aidha, ameongeza kuwa Serikali itasimamia mazingira sawa kwa kila chama kuendesha shughuli zake za kisiasa ikiwemo mikutano ya hadhara bila ubaguzi.