Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimefungua kesi dhidi ya Serikali katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kupinga zuio la mikutano ya hadhara ya kisiasa nchi nzima.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliwaambia waandishi wa habari kuwa katika kesi hiyo, wanawashitaki Kamanda wa Polisi wilaya ya Geita, Kamanda wa Polisi wilaya ya Kahama, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa polisi (Makao Makuu) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutoa maamuzi ambayo yanakiuka sheria na  demokrasia ya vyama vingi nchini.

Katika kesi hiyo, Chadema wameweka wanasheria watatu ambao ni Gasper Mwanalyela, John Mallya na Paul Kipeja.

“Tunaiomba mahakama itangaze amri ya jeshi la polisi ya kuzuia mikutano ya vyama vya siasa ni batili, utekelezaji unaofanywa ni batili, polisi wapewe tangazo la kutowanyanyasa wapinzani na pia itoe amri ya vyama vya siasa kufanya mikutano yake na polisi wawe walinzi wa mikutano hiyo,” alisema Mbowe.

Hivi karibuni, Jeshi la Polisi lilizuia mikutano yote ya hadhara ya kisiasa nchini hadi pale itakapotangaza vinginevyo kutokana na hali ya kiusalama. Jeshi hilo lilisambaratisha mkutano wa Chadema Wilaya ya Kahama kutokana na kutaka kufanyika licha ya kupokea barua ya polisi kuwazuia iliyotoka saa chache baada ya ile ya kuwapa kibali cha kufanya mkutano huo.

Ole Medeye aikimbia Chadema, amtetea Naibu Spika
Basi la Mwendokasi lamuua Mlemavu