Meneja wa klabu bingwa nchini England, Leicester City Claudio Ranieri, amesema anatafuta njia ya kumsaidia kiungo mshambuliaji Riyad Mahrez, ambaye kwa sasa anakabiliwa na wakati mgumu wa kuiwezesha klabu hiyo kufanya maajabu kama ilivyokua msimu uliopita.

Mahrez ambaye alimaliza msimu wa 2015/16 kwa kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa chama cha wachezaji wa kulipwa nchini England (PFA Player of the Year), amekua na changamoto ya kushindwa kutoa msaada dhidi ya wachezaji wengine kutokana na upinzani anaokutana nao kutoka kwa timu pinzani.

Ranieri, amesema kwa sasa anatafuta mbinu itakayomuwezesha kiungo huyo kurejea kwenye uwezo wake wa kucheza soka kwa kuzikabili changamoto zilizopo.

“Nitalazimika kusaka mbinu mbadala za kumsaidia, kwa sababu wapinzani wetu wamekua wanatukamia kila tunapocheza, hali ambayo inasababisha baadhi ya wachezaji wangu kuwa na wakati mgumu wa kuonyesha uwezo wao hususan Mahrez.

“Kama unafuatilia vizuri michezo yetu, Mahrez amekua na changamoto kubwa kuliko wachezaji wengine, kutokana na ufahamu wa timu pinzani kutambua amekua chanzo cha kupeleka mashambulizi.”

“Nimejaribu kumsihi acheze kwa uangalifu, lakini bado mambo yanaendelea kumuhelemea zaidi anapokua kwenye majukumu, kwa hiyo sina budi kumlinda mchezaji huyu ambaye ana viwango vyenye ubora wa kipekee.” Alisema Ranieri.

Mwishoni mwa juma lililopita Mahrez, alifunga bao la kufutia machozi kwa mkwaju wa penati katika mchezo wa ligi kuu ya England dhidi ya Watford ambao walichomoza na ushindi wa mabao mawili.

Leicester City kwa sasa wanaendelea kusota katika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi ya England na huenda mambo yakawa magumu sana msimu huu, kutokana na ushindani mkubwa unaoendelea kuonekana.

Lembeli awachongea vigogo wa Serikalini kwa Magufuli
Bashe: Mfumo wa kupata viongozi ndani ya CCM ni gulio