Aliyekuwa Mbunge wa Kahama Mjini, James Lembeli amesema kuwa vita dhidi ya ujangili nchini haitafanikiwa kwani baadhi ya vigogo waliopewa dhamana hiyo ndio wanaoihujumu.

Lembeli amedai kuwa ni kama Rais Magufuli anapigana vita hiyo peke yake kwani amesimama katikati ya watu waliokuwa wakihujumu juhudi hizo hapo awali.

“Katika vita hii dhidi ya ujangili, Rais Magufuli yuko peke yake kwa sababu amesimama katikati ya waliozoea kula kutokana na kushiriki au kusaidia ujangili,” Lembeli anakaririwa na Mwananchi kupitia mahojiano maalum yaliyofanyika hivi karibuni jijini Mwanza.

Mwanasiasa huyo ambaye alikihama Chama Cha Mapinduzi na kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo miezi michache kabla ya kuanza mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka jana, aliwahi kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira akijipatia umaarufu zaidi kwa kuongoza kamati iliyoibua sakata la ‘oparesheni tokomeza’.

Lembeli amemshauri Rais Magufuli kutekeleza mapendekezo ya Kamati yake kuhusu sakata la ‘Oparesheni Tokomeza’ lakini pia ateue watu kutoka nje ya mfumo wa Serikali na vyombo vya dola na kwamba awalinde. Alisema mambo hayo mawili yatamsaidia Rais Magufuli kufanikisha dhamira yake ya kutokomeza ujangili nchini.

Aitor Karanka Aelezea Alivyoikataa Chelsea FC
Claudio Ranieri Kumnoa Kivingine Riyad Mahrez