Mkuu wa Wilaya ya Momba, Fakii Lulandala ameahidi kutoa ekari 200 za ardhi bure kwaajili ya ujenzi wa Kiwanda cha kuchakata mazao kitakacho milikiwa na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB).
Akizungumza Mkoani humo hii leo April 26, 2023 Fakii amesema endapo CPB itajenga kiwanda hicho katika eneo hilo itasaidia kuinua Uchumi wa Wananchi ambao ni wakulima wa ukanda huo kwani watapata soko la uhakika la kuuza mazao yao.
“CPB hapa mmefika, kuna eneo la hekari mia mbili nawapa bure mje kuwekeza kiwanda hapa, naamini uwekezaji huo utainua Uchumi wa mtu mojamoja na hata Serikali kwa Ujumla,’’ amesema Lulandala.
Aidha ameongeza kuwa, mazao yanayolimwa kwa wingi Wilayani hapo ni pamoja na Mahindi, Mpunga na Maharage hivyo anaamini uwekezaji wa kiwanda Wilayani hapo utasaidia kuinua Uchumi wa Wakulima kwani wakulima hao watapata soko la uhakika kwa bei ya soko.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya CPB, Salum Awadh amesema yuko tayari kutuma watu wakafanye tathmini katika eneo hilo kama linafaa kujenga kiwanda cha kuchakata mazao huku akisema, ’natoa agizo viongozi wa CPB wataenda kuliangalia eneo hilo na kufanya tathmini tukijiridhisha tutakuja kujenga Kiwanda cha kuchakata mazao Wilayani Momba’’, amesema Awadhi
CPB imetenga Sh. Billioni 100 kwaajili ya kununua mazao na uwekezaji wa viwanda katika maeneo mbalimbali hapa nchini katika mwaka wa fedha 2023/2024.