Katika Serikali ya awamu ya tano kumezuka tabia kwa baadhi ya wakuu wa wilaya na wakuu wa mkoa kutumia madaraka yao ovyo kwa kuwaweka mahabusu watumishi wa umma kwa makosa ya kitaaluma.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amekemea vikali tabia hiyo na kusema kwamba kwa kufanya hivyo kunawupunguzia morali na nguvu watumishi hao kufanya kazi.
Na amewataka wakuu wa mkoa na wakuu wa wilaya kuacha mara moja tabia hiyo, amesema kuwa endapo makosa kama hayo yakijitokeza yashughulikiwe na mamlaka wanazofanyia kazi.
“Nakushukuru mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo sijawahi kusikia umefanya kitendo cha namna hiyo. Ukiona makosa ya kitaaluma walete juu tutawashughulikia,” amesema Ummy.
Ummy amezungumza hayo wakati akizindua jengo la wodi ya wazazi na matibabu ya dharura katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo yaliyojengwa kwa udhamini wa Taasisi ya Dhi Nureyn.
Hata hivyo Waziri Ummy bado hajabainisha wazi mwarobaini wa wakuu wa wilaya na mkoa watakokaokiuka agizo hilo.
Hata hivyo agizo hilo limekuwa likitolewa mara kwa mara na baadhi ya viongozi wakiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene na Naibu waziri wa wizara hiyo, Selemani Jafo, kuwaonya wakuu hao kutumi vizuri sharia inayowaruhusu kuwaweka ndani watu katika maeneo yao.