Amesema kuwa kukifungia chuo pekee haitoshi wanatakiwa kurudisha fedha zote za ada walizolipwa na wanafunzi katika mwaka huo wa masomo uliopita ili kuwasaidia kulipa vyuo vingine.
“Kuwarudishia fedha sio mwisho wa jambo hili kwa sababu mmepotezewa muda wenu na haki yenu ,mmeonewa, mmedhulumiwa kwa kusema hivyo namwagiza Mkuu wa Polisi wa Wilaya na timu yake kuwakamata sasa hivi na wafikishwe kwenye vyombo vya kisheria ili haki iweze kutendeka,” alisema Ndejembi.
Amewataja wanaotakiwa kuchukuliwa hatua za kisheria kuwa ni mmiliki wa chuo hicho Mathew Nkurlu, Msajili wa Chuo Yohana Michael, Mhasibu Elieth Ruben, wakufunzi Pendael Petro na Christopher Mabatian.
Ndejembi ametaja sababu za kuagiza wakamatwe viongozi hao wa chuo ni kuwa walihusika kushiriki katika kufanya udanganyifu na kuwatapeli wanafunzi hao huku wakijua kinachoendelea.
Aidha, ameongeza kuwa serikali itawasaidia wanafunzi hao kufanya utaratibu wa kupata vyuo vingine kwa wale wenye sifa za kujiunga na vyuo katika kozi ambayo walianza kusoma, hata hivyo amesema kama ikitokea chuo hicho kikakosa fedha za kuwarudishia wanafunzi hao, majengo yao yatatumika kama dhamana ya ada kwa vyuo ambavyo vitawapokea wanafunzi.