Kiungo Dele Alli huenda akakosa michezo ya awali ya fainali za kombe la dunia, endapo England itafanikiwa kufuzu kucheza fainali hizo, zitakazounguruma nchini Urusi mwaka 2018.

Dele yupo hatarini kufungiwa na shirikisho la soka duniani FIFA, kufuatia kitendo cha kuonyesha kidole cha kati wakati wa mchezo wa kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia dhidi ya Slovakia uliochezwa usiku wa kuamkia leo. Inahisiwa Dele alikua amekusudia kumtusi mwamuzi, kutokana na kukerwa na maamuzi yake dhdi ya kikosi cha The Three Lions.

Kitendo hicho hakikuonwa na mwamuzi Clement Turpin kutoka nchini Ufaransa, na kimechukua nafasi kubwa katika vyombo vya habari, kutokana na picha zilizopigwa na waandishi wa habari waliokua wanafuatilia mpambano huo uliomalizika kwa England kupata ushindi wa mabao mawili kwa moja.

Hata hivyo Dele amesema hakua na kusudio ovu kama inavyochukuliwa na kuelezwa katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, bali alifanya hivyo ikiwa ni ishara ya kumtania aliyekua mchezaji mwenzake wa Spurs Kyle Walker ambaye kwa sasa anaitumikia Man city.

Dele  mwenye umri wa miaka 21, tayari ameshawaomba radhi wadau wa soka waliokipokea kwa hisia mbaya kitendo hicho, kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, na ameendelea kusisitiza hakua na nia mbaya.

“Ishara wa kidole niliyoionyesha usiku huu, ilikua ni muendelezo wa utani kati yangu na Kyle Walker! Ninaomba radhi kwa yoyote aliekwazika na tukio hilo! Ameandika Dele kwenye ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Twitter.

Kwa upande wa kocha mkuu wa kikosi cha England Gareth Southgate aliwaambia waandishi wa habari kuwa: “Sikuona kitendo kama hicho, lakiini itanibidi nifuatilie kwa umakini. Najua Kyle na Dele ni watu wanaopenda kutaniana kila wakati. Kwa hiyo siwezi kuhukumu moja kwa moja kama Dele alifanya kitendo hicho kwa kumkusudia Kyle.

Shirikkisho la soka duniani FIFA, linatarajiwa kufuatilia kwa kina kitendo hicho kupitia kamati yake ya nidhamu, na kama watabaini kiungo huyo alikusudia kumtusi mwamuzi Turpin, huenda wakamfungia michezo minne.

Kufuatia ushindi wa usiku wa kuamkia leo dhidi ya Slovenia, England imejiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu kucheza fainali za kombe la dunia za 2018, na kama adhabu itatolewa kwa Dele, haitoingilia michezo ya kimataifa ya kirafiki.

Diane Rwigara atiwa mbaroni
Wabunge wa upinzani wasusia bunge