Meneja wa klabu ya West Ham Utd Slaven Bilic kwa mara ya kwanza amezungumza hadharani kuhusu tofauti zilizojitokeza kati yake na kiungo mshambuliaji kutoka nchini Ufaransa Dimitri Payet.

Bilic amezungumza tofauti zilizopo akiwa katika mkutano na waandishi wa habari, ambapo amesema mchezaji huyo amegoma kuichezea The Hammers kwa shinikizo la kutaka kuondoka katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili.

Meneja huyo kutoka nchini Croatia amesema Payet alisusia mazoezi ya kujiandaa na mchezo wa ligi kuu ya soka nchini England wa mwishoni mwa juma hili, ambapo watapambana na Crystal Palace.

Hata hivyo Bilic amesisitiza kuwa, West Ham Utd haipo tayari kumuuza Payet licha ya jambo hilo kutokea katika kipindi hiki ambacho wachezaji wanaruhusiwa kuhama kutoka klabu moja kwenda nyingine.

Amesema dhamira yake ni kutaka kuona Payet anaendelea kubaki klabuni hapo, na anaamini suala hilo litapatiwa ufumbuzi kwa njia ya mazungumzo.

Tayari uongozi wa West Ham Utd umeonyesha nia ya dhati ya kutaka kuendelea kufanya kazi na Payet, na mwaka 2016 walikuwa katika mazungumzo ya kumsainisha mkataba wa miaka mitano, ambao utamuwezesha kulipwa mshahara wa Pauni 125,000 kwa juma, lakini jambo hilo halijafanikiwa mpaka sasa.

Payet amekua anahusishwa na taarifa za kuwindwa na baadhi ya klabu za barani Ulaya, tangu alipoonyesha kiwango cha hali ya juu msimu uliopita, huku nyota yake iking’aa kwenye fainali za mataifa ya Ulaya (Euro 2016) zilizofanyika nchini Ufaransa.

Ben Pol: Thamani ya Sauti yangu ni zaidi ya millioni 10
JPM: Wakulima pandisheni bei mtakavyo