Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri Namibia zimesaini Hati za Makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya Usalama, Nishati na Mashauriano ya Kisiasa na Kidiplomasia.

Hati za Makubaliano hayo zimesainiwa katika Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JCC) kati ya Tanzania na Namibia uliomalizika jijini Windhoek, Namibia tarehe 10 Machi 2023 katika ngazi ya Mawaziri.

Mkutano huo wa tatu wa JCC kati ya Tanzania na Namibia umejadili na kutathimini masuala mbalimbali ya utekelezaji kwenye maeneo ya ushirikiano yaliyokubaliwa baina ya nchi hizi.

Maeneo hayo ni pamoja na Siasa na Diplomasia, Ulinzi na Usalama, Uchumi, Nishati, Kilimo, Maendeleo na Miji, Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Maliasili, Utalii na Mazingira, na Uvuvi, Afya, Elimu na Utamaduni.

Aidha, mkutano huu wa Mawaziri umewaagiza watendaji katika sekta za ushirikiano kukamilisha kwa wakati masuala yote yanayohitaji utekelezaji ndani ya muda ulioazimiwa na kikao hicho ili kuleta tija katika shughuli za wananchi na kuwainua kiuchumi.

Wakihutubia katika ufunguzi wa mkutano huo Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na Namibia Dkt. Stergomena Tax na Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah wamesisitiza umuhimu wa kukuza mawasiliano baina nchi hizo mbili ili kuweza kurithisha kizazi cha sasa juu ya historia ya mataifa hayo mawili na kufahamu ndoto kubwa waliyokuwa nayo waasisi wa matifa haya katika kuyafikia maendeleo ya watu wake.

Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Mkutano huu umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax ambaye ameambatana na Naibu Waziri Wizara ya Mifugo na Uvuvi, David Silinde na Naibu Waziri Wizara ya Nishati, Steven Byabato.

Mila potofu zinaharibu ndoto za walio wengi: Mbunge Tawfiq
Teknolojia, mikopo nafuu yasaidia mapambano ukatili wa kijinsia