Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ametoa katazo kwa kampuni zinazosimamia na kutekeleza miradi ya umeme nchini, kutonunua nje ya nchi vifaa vya umeme ambavyo vinazalishwa nchini, ili kukuza viwanda vya ndani vinavyozalisha vifaa hivyo, kuvipa thamani, kukuza ajira na uchumi wa nchi.

Dkt. Biteko ametoa agizo hilo hii leo Novemba 15, 2023 Mkoani Mtwara, wakati alipokagua miradi ya umeme vijijini na kuwasha umeme katika Kata ya Naliendele, eneo la Pachota A na Kijiji cha Nachenjele.

Amesema, “TANESCO na REA, tabia ya kununua vifaa vya umeme nje ya nchi hiyo ni zilipendwa, viwanda vipo ndani ya nchi halafu vifaa vinanunuliwa nje, hivi vifaa vyetu mnataka tukauze wapi, kuanzia leo na kuanzia nilivyoingia ndani ya ofisi lazima bidhaa zinazozalishwa hapa zinunuliwe na vifaa visivyopatikana ndani ya nchi ndio viagizwe  kutoka nje, tukuze viwanda vyetu, tuvipe thamani na kukuza ajira.”

Aidha, Dkt. Biteko amewataka wakandarasi wa umeme vijijini kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi na kueleza kuwa Serikali itafanya tathmini ya kila mkandarasi kuona alivyotekeleza miradi na ambao hawafanyi vizuri watasitishiwa mikataba kwani Serikali inalipa wakandarasi hao na itaendelea kuwalipa hivyo hawana sababu za kukwamisha Miradi ya Upelekaji Umeme Vijijini.

“Angalieni mabilioni yaliyomwagwa kwenye Mkoa wa Mtwara, shilingi bilioni 170 zimeletwa hapa kusambaza umeme vijijini ambazo zitafaidisha pia maeneo ya mijini lakini yanafanana na kijijini, lengo letu ni mwezi wa sita mwakani kumaliza kazi ya kupeleka umeme vijijini na kuhamia vitongojini.” Amesema Dkt. Biteko

Pamoja na kuwapongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kusimamia vyema kazi ya kusambaza umeme, amewataka kutokucheka na wakandarasi hao ili kazi ya kupeleka mahitaji ya umeme kwa wananchi ifanyike kwa ufanisi.

Victor Osimhen afunguka alivyoitosa Al Hilal
Adel Zrane akaribia kutua Simba SC