Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, DkT. Hussein Ali Mwinyi amezitaka Taasisi za Serikali na Jumuiya zote za waajiri na waajiriwa kuhakikisha wanawasilisha michango katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar – ZSSF, kwa wakati.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo katika kilele cha maadhimisho ya miaka 25 ya Mfuko huo na kuzindua mradi wa Mji wa Dkt. Hussein Ali Mwinyi uliopo Mombasa Zanzibar pamoja na Mfumo wa Huduma kwa Wateja wa kuwasiliana wa ZSSF WhatsApp, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Aidha, Rais DkT. Mwinyi pia amewashauri wajasiriamali wote kujisajili na kuchangia Mfuko wa Hiari kupitia mfuko huo kwani una faida kubwa kwa biashara zao na kusisitiza kuwa uwasilishaji wa michango katika mfuko wa ZSSF, utarahisisha shughuli za uendeshaji wa mfuko huo katika kuwajengea misingi mizuri wafanyakazi wao wanapostaafu.
Hata hivyo, amewapongeza ZSSF kwa kuanza kulipa mafao mapya mawili kwa wanachama wake waliopoteza ajira na walioumia wakiwa kazini na kuwahimiza kuendelea kuzingatia utekelezaji wa agizo lake alilolitoa siku ya Wafanyakazi Mei Mosi 2023 la kuongezeka kwa malipo ya pensheni kwa wastaafu.