Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amewataka Watumishi wa Umma nchini kuutumikia umma kwa uzalendo, uadilifu na weledi ili kutimiza azma ya Serikali ya kutoa huduma bora kwa wananchi.

Amesema hayo wakati akifungua kikao kazi cha siku mbili cha taasisi simamizi za maadili na vyama vya kitaaluma chenye lengo la kubadilishana uzoefu wa usimamizi wa maadili, kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI jijini Dodoma.

“Ushirikiano uliopo kati ya ofisi yangu na taasisi simamizi za maadili na vyama vya kitaaluma, utasaidia kujenga uadilifu kwenye utumishi wa umma na jamii kwa ujumla”, amesema Dkt. Ndumbaro .

Amesema kuwa watumishi wa Umma nchini wanao wajibu wa kuunga mkono kwa vitendo azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuujenga Utumishi wa Umma kuwa wenye kuzingatia uadilifu, uwajibikaji, Kanuni, Sheria, Taratibu na miongozo iliyopo.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Maadili, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Leila Mavika amesema lengo kuu la kikao kazi hicho ni kukumbushana uzingatiaji wa maadili, kujadili changamoto za usimamizi wa maadili katika Utumishi wa Umma na kuzitafutia ufumbuzi.

Mwanasheria wa Bodi ya Wataalamu ya Ununuzi na Ugavi, Suleiman Mzava ambaye ni mmoja wa washiriki wa kikao kazi hicho amesema, kikao kazi hicho kitasaidia kujenga uadilifu miongoni mwa taasisi za umma hivyo ameipongeza Serikali kwa kuweka nguvu kubwa katika usimamizi wa maadili.

.

Muhagama asisisitiza mifumo ya usalama na afya kuboreshwa
Oscar Oscar aishangaa TFF, TPLB