Waziri wa Habari wa Eritrea, Yemane Meskel amesema nchi yake imejiunga tena na Jumuiya ya Afrika Mashariki -IGAD, ikiwa ni karibu miaka 16 baada ya taifa hilo lililojitenga kisiasa kujiondoa kutoka kwa Jumuiya hiyo.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Meskel ameandika kuwa Taifa hilo la Eritrea, limeanza tena shughuli zake katika IGAD na kuchukua kiti chake katika mkutano ulioandaliwa na jumuiya ya mataifa saba nchini Djibouti.
Alieleza kuwa, nchi hiyo iko tayari kufanya kazi kuelekea amani, utulivu, na ushirikiano wa kikanda. Nchi hiyo ya kiimla ilisitisha uanachama wake wa IGAD mwaka 2007 kufuatia msururu wa kutoelewana, ikiwa ni pamoja na uamuzi wa Umoja huo kuitaka Kenya kusimamia utatuzi wa mzozo wa mpaka, kati ya Ethiopia na Eritrea.
Eritrea ilijitenga na Ethiopia mwaka 1993 na kupigana vita vya mpakani vya miaka miwili na jirani yake ambavyo vilitia sumu mahusiano pamoja na makubaliano ya amani mwaka 2018 na kufuatia ushirikiano na Addis Ababa, wanajeshi wa Eritrea waliunga mkono vikosi vya Ethiopia wakati wa vita vya serikali kuu dhidi ya Tigray People’s Liberation Front – TPLF.