Mshambuliaji hatari wa Mabingwa wa Soka nchini England Manchester City, Erling Haaland amesema watafanya juu chini wabebe makombe matatu msimu huu.

Tayari Man City imebeba ubingwa wa Ligi Kuu England na itaongeza kombe la pili endapo itaifunga Manchester United leo kwenye fainali ya Kombe la FA.

Baada ya mchezo huo, Man City itajiandaa na fainali nyingine ya michuano ya Ligi Mabingwa Ulaya dhidi ya Inter Milan itakayochezwa Juni 10 katika Jiji la Instabul, Uturuki.

Man City inataka kutengeneza historia iliyowekwa na Man United 1999 ilipobeba FA, Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ligi Kuu England.

Haaland alisema itakuwa na mafanikio makubwa kama historia hiyo ikijirudia, lakini kwa upande wa Man City inayolewa na kocha Pep Guardiola.

Licha ya Man City kutawala makombe ya ndani ya ligi haijawahi kubeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya katika historia ya klabu hiyo, huku Haaland akiwa na matumaini ya kulinyakua msimu huu.

“Hii ndio maana (Man City) wamenisajili. Nimekuja hapa kwa ajili ya kubeba makombe. Itamaanisha kila kitu kwangu nifanye juu chini. Nitajaribu kuisaidia timu naamini ndoto zangu zitatimia. Hata hivyo haitakuwa rahisi ni fainali mbili dhidi ya timu mbili nzuri. Tutapambana na kuzifunga,” amesema.

Haaland amevunja rekodi ya ufungaji wa mabao mengi msimu huu baada ya kufunga 52 na kutunukiwa tuzo kadhaa katika mashindano hayo.

Mchezaji huyo ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka iliyoandaliwa na waandishi wa habari wa michezo (FWA).

Pia, straika huyo wa kimataifa wa Norway ndiye mchezaji wa kwanza kushinda tuzo hiyo. Nyingine ni ile ya chipukizi bora wa mwaka.

Mtibwa Sugar: Tunazitaka alama zote sita
Ikulu yatafafanua kilichomuangusha Rais jukwaani