Hofu imetanda kwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Italia, Antonio Conte baada ya mshambuliaji Graziano Pelle kuondoka mazoezini akiwa anachechemea hapo jana kufuatia maumivu ya goti.

Conte alionekana kuwa katika hali ya kustaajabu kufuatia tatizo hilo, ambalo lilisababishwa na mgongano uliojitokeza kati ya Pelle na mchezaji mwenzake wakiwa katika mazoezi.

Mshambuliaji huyo wa klabu ya Southampton, amekua akisumbuliwa na goti kwa muda mrefu, hali ambayo ilimsababishia kukosa kucheza michezo minne kwa kipindi cha mwezi mmoja, kabla ya kurejea katika michezo ya mwisho ya ligi ya nchini England na kufunga mabao sita.

Hata hivyo kabla ya kutonesha maumivu ya goti, mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 30, alikuwa katika muendelezo mzuri wa kutimiza majukumu yake uwanjani, na katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita aliifungia Italia bao moja na la ushindi dhidi ya Scotland.

Endapo itathibitika Pelle ameumia na kufikia hatua ya kushindwa kucheza katika fainali za Euro 2016, kocha wa Italia Antonio Conte atalazimika kufanya maamuzi ya kumtumia mmoja kati ya washambuliaji wengine waliopo kikosini kama Eder (Inter Milan), Ciro Immobile (Torino), Lorenzo Insigne (Napoli) pamoja na Simone Zaza (Juventus).

Wakati huo huo mlinda mlango namba moja wa Italia Gianluigi Buffon, naye alikosa mazoezi ya jana kufuatia maumivu ya misuli ya paja yanayomkabili.

Italia imepangwa katika kundi E, na itaanza kupapatuana na Ubelgiji Juni 13, kisha Sweden (Jini 17) na itamaliza michezo ya kundi hilo kwa kupamba na Jamuhuri ya Ireland, Juni 22.

Kabla ya kuelekea nchini Ufaransa, kikosi cha Italia kitacheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki wa mwisho dhidi ya Finland siku ya jumatatu ya juma lijalo.

Euro 2016: Pele Amtumia Salamu Marcus Rashford
Rais Shein awafyatua CUF, asema hawezi kuondolewa madarakani kwa kuroga