Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein amewatumia ujumbe wapinzani wake wa Chama Cha Wananchi (CUF) kuwa kamwe hataondoka madarakani kwa kupelekwa kwa waganga wa kienyeji na kurogwa.

Dk. Shein alituma ujumbe huo alipozungumza na wafuasi wa CCM katika Tawi la Wesha Shengejuu, tawi ambalo linadaiwa kuchomwa moto na wafuasi wa CUF.

“Mkipata nafasi waambieni wapinzani kwamba nchi haiwezi kuondolewa madarakani kwa kufanya uganga wa kienyeji na kuroga,” alisema.

Kauli hiyo ilikuja baada ya baadhi ya makada wa CCM kumueleza kuwa baadhi ya viongozi na wafuasi wa CUF wamekuwa wakikesha kwa waganga wa kienyeji wakitafuta jinsi ya kuiondoa madarakani Serikali yake.

Dk. Shein alieleza kuwa Serikali yake ipo kihalali kwa mujibu wa sheria kwa kuwa ilichaguliwa katika uchaguzi wa Marudio uliofanyika Machi 20 mwaka huu baada ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kufuta uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana.

Aliwataka wanachama wa chama hicho kutokuwa na wasiwasi na kutopotoshwa na maneno ya wapinzani huku akiahidi kulijenga upya Tawi hilo lililochomwa moto.

CUF, wamekuwa wakipinga Serikali ya Dk. Shein ambapo hivi karibuni Katibu Mkuu wa Chama hicho ambaye alikuwa mgombea urais katika kinyang’anyiro cha uchaguzi uliopita amekuwa akikaririwa akidai Serikali hiyo itaondoka madarakani kwa amani kwa presha ya wananchi kabla ya mwaka 2020.

Euro 2016: Graziano Pelle Azua Hofu Kambi Ya Italia
Wabunge wa Upinzani wamsusia tena Naibu Spika