Mshambuliaji Radamel Falcao, hana nafasi kubwa ya kuendelea kukaa Stamford Bridge yalipo makao makuu ya klabu ya Chelsea, kwani huenda akaondoka mwezi januari mwaka 2016.

Mshambuliaji huyo kutoka nchini Colombia, alipewa nafasi kubwa ya kuitumikia klabu hiyo ambayo inashikilia taji la ubingwa nchini England, baada ya kusajiliwa mwanzoni mwa msimu huu, lakini imeonekana mambo kumuendea tofauti chini ya utawala wa meneja Jose Mourinho.

Mpaka sasa Falcao ameshacheza michezo saba akiwa na klabu hiyo na amefunga bao moja, hali ambayo imempotezea imani Mourinho pamoja na mashabiki wa Chelsea, ambao waliamini wamepata mshambuliaji ambaye angekua mbadala wa Didier Drogba aliyeondoka klabuni hapo mwishoni mwa msimu uliopita.

Falcao, anapigiwa chapuo la kurejeshwa kwenye klabu yake ya AS Monaco ambayo imekua ikimtoa kwa mkopo tangu msimu uliopita alipokwenda Man Utd na sasa yupo Chelsea.

Akiwa Man Utd msimu uliopita, Falcao mwenye umri wa miaka 29, alicheza michezo 29 na kubahatika kufunga mabao 4 pekee.

Rejesha Furaha Na Amani Katika Uhusiano Wako, Fuata Njia Hizi Kumi
Ajira Ya Tim Sherwood Yaning'inia