Kiungo kutoka nchini England na klabu ya New York City FC, Frank James Lampard amesema hana uhakika kama msimu ujao wa michuano ya Ligi Kuu Marekani (MLS), utakuwa wa mwisho kwake kusakata kandanda.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 37, ameonyesha shaka ya kuwepo ama kutokuwepo katika soka kuanzia msimu ujao wa ligi, kufuatia majeraha ambayo yalimuweka nje ya uwanja katika msimu wake wa kwanza alipokwenda nchini Marekani.

Kwa sasa Lampard, anajiandaa kucheza msimu wake wa pili tangu alipojiunga na klabu ya New York City FC, akitokea nchini kwao England ambapo alimalizana na klabu ya Chelsea ambayo ilimuhodhi kwa muda wa miaka 14.

Lampard alibahatika kurejea nchini England kuitumikia klabu ya Man city, lakini alipatwa na majeraha ya kiazi cha mguu, halia mbayo iliibua wasiwasi wa kuendelea kucheza soka akiwa na klabu yake mpya huko nchini Marekani.

Hata hivyo kwa sasa Lampard anajifua vyema na New York City chini ya meneja kutoka nchini Ufaransa, Patrick Vieira akiwa anajiandaa kuivaa Chicago Fire, mtanange utakaopigwa Machi 6, mwaka huu.

Lampard anasema hafahamu kitakachomtokea.   “Sifahamu kama huu utakuwa mwaka wangu wa mwisho kucheza soka.” Lampard aliliambia gazeti la Daily Mail. “Hata kama itakuwa hivyo ama hapana, sitaki kumaliza soka nikiwa vibaya,” aliongeza nyota huyo.

Guus Hiddink Ang'aka Kuhusu Ratiba Ya FA, Champions League
Sakata La Kashfa Za Jerry Muro, Manara Abisha Hodi Kwa Waziri Nape