Meneja wa muda wa klabu ya Chelsea, Guus Hiddink amelalamikia ratiba ya mchezo wa kombe la chama cha soka nchini England FA, ambapo The Blues watapambana na Everton, ikiwa ni siku tatu baada ya mchezo wao wa mkondo wa pili wa hatua ya 16 bora wa ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya Paris Saint Germain kutoka nchini Ufaransa.

Hiddink amelelemikia ratiba hiyo, kwa kuhofia wachezaji wake ambao atalazimika kuwatawanya katika makundi mawili ili aweze kutimiza lengo la kupambana katika michezo yote miwili na kufanikisha azma ya ushindi.

Amesema kuna wasiwasi mkubwa wa wachezaji wake wa kikosi ambacho atakitumia katika mchezo wa kombe la FA wakapata dhoruba endapo atawatuimia katika mchezo wa ligi ya mabingwa barani Ulaya.

Hata hivyo meneja huyo kutoka nchini Uholanzi, amesema hana budi kupambana na kupanga mbinu mbadala ambazo zitamsaidia katika michezo hiyo muhimu kwake pamoja na kwa klabu ya Chelsea.

Tayari Hiddink ana wasiwasi wa kumkosa mshambuliaji kutoka nchini Hispania, Pedro Rodrigues katika moja ya michezo hiyo miwili, baada ya kuumia misuli ya paja mwishoni mwa juma lililopita wakati wa mchezo wa ligi ya nchini England ambapo Chelsea walichomoza na ushindi wa mabao mawili kwa moja.

Chelsea, watapambana na PSG March 09, katika mchezo wa mkondo wa pili wa hatua ya 16 bora wa ligi ya mabingwa barani Ulaya na kisha watarejea uwanjani March 12 kupambana na Everton kwenye mpambano wa kombe la FA.

Mbali na michezo hiyo, kesho Chelsea watakabiliwa na mchezo mwingine wa ligi ya nchini England dhidi ya Norwich City, kwenye uwanja wa Carrow Road mjini Norwich.

Kompany Atoa Ya Moyoni Kuhusu 2014-15
Frank Lampard Ajipigia Hesabu Kustaafu Soka