Klabu ya New York City FC imethibitisha taarifa za kutosaini mkataba mpya na kiungo kutoka nchini England Frank Lampard, mara baada ya mkataba wake wa sasa utakapofikia kikomo.

Lampard, mwenye umri wa miaka 38, alijiunga na klabu hiyo inayoshiriki ligi ya nchini Marekani (MLS) mwaka 2014, na amekua na wakati mgumu wa kucheza mara kwa mara kutokana na kukabiliwa na majeraha.

Tangu alipotua klabuni hapo, Lampard amefanikiwa kufunga mabao 15 katika michezo 31 aliyocheza.

Kwa ujumla kiungo huyo ameweka rekodi ya kufunga mabao 300 katika michezo 1,000 aliyocheza tangu alipoaanza kucheza soka la kulipwa mwaka 1994 akiwa na klabu ya West Ham Utd na kisha alijiunga na Chelsea mwaka 2001 kabla ya kutimkia nchini Marekani.

“Wakati wangu wa kucheza soka nikiwa na klabu ya NYCFC unakaribia kufika mwisho kikomo, sina budi kuwashukuru watu wote wanaohusika na klabu hii kwa ukarimu wao walionionyesha tangu nilipofika hapa miaka miwili iliyopita.” Alisema Lampard.

Katika hatua nyingine meneja wa klabu hiyo iliyo na maskani yake makuu mjini New York, Patrick Vieira amezungumza hatua ya kuondoka kwa Lampard.

“Kila mmoja anamzungumza Frank kuhusu kasi ndogo ya ufungaji wa mabao tangu alipofika klabuni hapa, lakini kwangu nimejifunza mambo mengi kumuhusu, kutokana na uwezo mkubwa waliouonyesha mbali na suala la mabao ambalo limechukua nafasi kubwa.

“Huenda ikawa imewakwaza watu wengi kuhusu uwezo wa kufunga kutokana na majeraha ya mara kwa mara, lakini kwa mwaka mmoja niliofanya kazi hapa, sina budi kumshukuru Lampard kwa kazi nzuri aliyoifanya na ninamtakia kila la kheri.” Alisema meneja wa NYCFC Patrick Vieira.

Klabu ya NYCFC ilitupwa nje ya michuano ya Conference katika hatua ya nusu fainali kwa kufungwa na Toronto mabao mawili kwa sifuri katika uwanja wa ugenini, na walipokwenda katika uwanja wao wa nyumbani walifungwa mabao matano kwa sifuri kwenye mchezo wa mkondo wa pili.

#HapoKale
Tim Howard Kusubiri Hadi Mwaka 2017