Mtangazaji wa kipindi cha Jahazi cha Clouds FM, Gardner G Habash amezungumza kwa masikitiko akimuelezea rafiki yake wa karibu, Empraim Kibonde aliyefariki dunia leo.
Gardner na Kibonde wamefanya kazi kwa miaka mingi kwenye kipindi cha Jahazi wakiwa pamoja kama mapacha kikazi, ambapo amemuelezea kwa sifa ambazo wengi tulikuwa hatuzifahamu ikiwa ni pamoja na elimu, ukwasi na mambo mengine.
Amesema kuwa rafiki yake hakupenda kujikweza lakini alikuwa na taaluma kubwa ya tasnia ya habari, mali na upeo mkubwa.
“Kibonde alikuwa hodari sana kwenye kazi anayoifanya, msomi amesoma masomo ya mambo haya ya mawasiliano na uandishi wa habari na amesoma mpaka nje ya nchi lakini bado alikuwa sio mtu wa kujikweza,” Gardner ameiambia Millard Ayo TV.
“Kibonde ni mtu ambaye ana mali lakini haoneshi kama ana mali, ni mtu ambaye ana uwezo sana lakini bado anajishusha kuwa mtu wa kawaida. Kwakweli kwenye tasnia ya habari alikuwa ni hodari sana.
“Mimi nimejifunza mambo kutoka kwake kwa sababu amenizidi kiumri ingawa tuko rika moja, na alianza kazi kabla yangu tangu enzi za CTN huko… kiumri amenizidi, kimasomo amenizidi, kiuzoefu amenizidi lakini nilikuwa nikifanya naye kazi anajionesha yeye yuko chini yangu,” Gardner aliongeza.
Alisema kuwa kwenye utangazaji yeye na marehemu Kibonde walikuwa wanamuunganiko mzuri zaidi hali inayomfanya kujiuliza, “sijui mimi nitafanya vipi kazi bila Kibonde.”
Kibonde alifariki akiwa anapatiwa matibabu jijini Mwanza kufuatia kuugua ghafla saa chache baada ya kutangaza kwenye msiba wa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, imeelezwa kuwa alipatwa na presha ghafla akiwa Bukoba.
Mungu Amrehemu, hakika tasnia ya habari imepata pigo lingine kubwa ndani ya kipindi cha wiki mbili tu, Ruge Mutahaba na Ephraim Kibonde. Wapumzike kwa amani.