Kampuni ya Sky Drive Inc ya nchini Japan imefanikisha jaribio lake la kwanza la kuendesha na kurusha gari linalopaa angani likiwa na mtu mmoja.
Katika video iliyowekwa mtandaoni mwishoni mwa wiki hii, kifaa hicho kinachoonekana kuwa na muundo wa pikipiki lakini kina ‘propellers’, kilipaa umbali wa kati ya mita 1-2 kutoka ardhini, kikifanya safari hiyo kwa dakika nne.
Mkuu wa Kampuni hiyo, Tomohiro Fukuzawa alisema kuwa jitihada zao zinawapa matumaini kuwa gari hilo linalopaa linaweza kuwa sio ndoto tena ifikapo mwaka 2023.
Hata hivyo, Fukuzawa alikiri kuwa kuhakikisha usalama wa chombo hicho ni zoezi lililokuwa gumu zaidi kwao.
“Kati ya miradi zaidi ya 100 duniani ya magari yanayopaa, ni hili moja tu ambalo limefanikiwa likiwa na mtu mmoja ndani yake,” Fukuzawa amewaambia waandishi wa habari.
“Tunatumaini kuwa watu wengi watahitaji kuliendesha na kujisikia furaha,” ameongeza.
Kwa sasa gari hilo linaweza kupaa kwa muda wa kati ya dakika tano hadi kumi, lakini kama litaweza kupaa kwa dakika 30, litakuwa na uwezo wa kufanya safari hata kutoka Japan kwenda China, kwa mujibu wa Fukuzawa.