Mara baada ya kusimamishwa kazi na Rais wa Nigeria, Bola Tinubu Gavana wa Benki Kuu ya Nigeria, Godwin Emefiele amefikishwa Mahakamani na kukana mashitaka ya kumiliki bunduki na risasi kinyume cha sheria.
Mawakili wa Serikali waliiomba Mahakama kuidhinisha kuzuiliwa kwa Emefiele kwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha na uvunjaji wa uaminifu wa jinai, mashtaka ambayo adhabu yake ni kifungo kirefu endapo yatathibitishwa.
Emefiele alijulikana kwa kutumia sera zisizo za kawaida ili kuweka sarafu ya naira ya nchi kuwa imara na kutoa mikopo ya moja kwa moja kwa biashara ili kujaribu kukuza ukuaji na aliwekwa kizuizini na idara ya usalama wa Taifa Juni 10, siku moja baada ya Rais mpya Bola Tinubu kumsimamisha kazi.
Hata hivyo, Mahakama ilimpa Emefiele dhamana kwa masharti ya kulipa naira milioni 20 na kusema anapaswa kuwekwa rumande hadi masharti ya dhamana yatakapotimizwa au hadi tarehe 14 Novemba kesi yake itakaposikilizwa.
Rais Tinubu, ambaye anaanza mageuzi kwa ujasiri katika nchi hiyo yenye uchumi mkubwa barani Africa katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja, Tinubu alikosoa sera za benki kuu ambayo ilikuwa chini ya Emefiele wakati alipoapishwa mwezi Mei, akisema walihitaji kusafisha nyumba vizuri.