Taarifa za awali kutoka Ufaransa zinaeleza kuwa Nahodha na Mshambuliaji wa kikosi cha Senegal Sadio Mane, atazikosa Fainali za Kombe la Dunia 2022 zitakazoanza baadae mwezi huu nchini Qatar.

Mane alipatwa na majeraha ya mguu jana Jumanne (Novemba 08) wakati wa mchezo wa Ligi ya Ujerumani ambapo Mabingwa watetezi FC Bayern Munich walikua nyumbani Allianz Arena wakicheza dhidi ya Werder Bremen.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 30, alipatwa na jeraha la mguu dakika ya 15 ya mchezo huo uliomalizika kwa Bayern Munich kushinda mabao 4-1, na nafasi yake kuchukuliwa na Leroy Sane.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Gazeti la L’Equipe la Ufaransa, Mshambuliaji huyo amefanyiwa vipimo na imebainika atakuwa nje ya Uwanja wa Kipindi kirefu kwa ajili ya kuuguza jeraha ya mguu.

Hata hivyo bado Klabu ya Bayern Munich haijatoa taarifa zozote kuhusu majibu ya vipimo alivyotarajiwa kufanyiwa Mane leo Jumatano (Novemba 08), kwa hiyo vyombo vya habari vinasubiri ili kuthibitisha ukweli wa kilichotangazwa na Gazeti la L’Equipe la Ufaransa.

Mane alitajwa kwenye kikosi wachezaji 26 kilichotangazwa jana Jumanne (Novemba 08) na Kocha Mkuu wa Senegal Aliou Cisse, na hatua ya kuumia kwenye mchezo wa jana wa Ligi Kuu ya Ujerumani inamfanya ajiunge na wachezaji wengine ambao wanahatihati ya kutokuwa kwenye safari ya kuelekea Qatar kwa sababu za kuwa majeruhi.

Wachezaji hao ni Edouard Mendy na Kalidou Koulibaly wanaoitumikia Klabu ya Chelsea pamoja na Idrissa Gueye wa Klabu ya Everton.

Wawili wa familia moja wafariki katika ajali
Rais akosoa wafadhili 'kuzibania' nchi masikini