Rais wa shirikisho la soka duniani FIFA Gianni Infantino ameendelea kuipa kipaumnbele kauli yake ya kutaka kuona fainali za kombe la dunia zinakua na timu shiriki 48.

Infantino alitumia kauli hiyo katika kampeni zake wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu wa FIFA, na baadhi ya nchi wanachama zilionyesha kuvutika na pendekezo hilo ambalo linapaswa kupitishwa na mkutano mkuu wa shirikisho hilo.

Infantino anaamini endapo pendekezo lake litapitishwa kwenye mkutano mkuu, fainali za kombe la dunia zitashuhudia makundi 16 ambayo yatakua na timu nyingi kutoka pande zote za dunia.

Mfumo huo mpya unadhihirisha katika kila kundi timu mbili zitakazomaliza katika nafasi ya juu zitatinga kwenye hatua mtoano, ambayo itashirikisha timu 32.

Infantino amesema angependa kuona mfumo huo unaanza kutumika katika fainali za kombe la dunia za mwaka 2026 endapo mkutano mkuu utaridhia pendekezo lake.

“Kila timu itakayofuzu kucheza fainali za kombe la dunia katika mfumo huu, italazimika kucheza angalau michezo miwili ya hatua ya makundi. Na timu mbili za kwanza zitafuzu kwenye hatua ya mtoano.” Alisema kiongozi huyo wa soka duniani.

Kwa sasa fainali za kombe la dunia zinashirikisha timu shiriki 32 ambazo huwekwa katika makundi manane, na timu mbili za juu katika kila kundi hufuzu kwenye hatua ya mtoano ya 16 bora.

Wamachinga waanza kurudisha vibanda vyao
Roy Hodgson: Ninajihisi Vizuri Zaidi Kuliko Nilivyokua