Baada ya subira ya muda mrefu, filamu ya iliyochezwa nchini Tanzania na Los Angeles, Marekani ikiwahusisha watanzania ya ‘Going Bongo’ ilianza kuoneshwa kwa mara ya kwanza katika jumba la Sinema la Cinemax Centuries, Jijini Dar es Salaam.

Filamu hiyo ya kitanzania ambayo mhusika wake mkuu ni Ernest Napoleone akicheza kama ‘Dk. Lewis Burger’ imeionekana kupata mafanikio katika wiki yake ya kwanza tangu ilipoanza kuoneshwa katika jumba hilo wiki iliyopita.

Mwandishi wa Dar24 alikuwa mmoja wa watazamani wa filamu hiyo Jumapili na kushuhudia watazamaji wakionesha hisia zao dhahiri za kukubali na kufurahishwa sana na filamu hiyo tangu ilipoanza hadi ilipomalizika.

Baada ya filamu hiyo, mwandishi wetu alipata nafasi ya kuongea na mhusika mkuu kwenye filamu hiyo kama shabiki wa filamu hiyo, Ernest Napoleone ambaye alieleza kuwa amefarijika kuona mwitikio wa watu na kwamba wengi wanaotoka wanaisifia.

Aliongeza kuwa ingawa filamu hiyo imeonesha kupata mafanikio, ameamua yeye na baadhi ya watu wake kuhudhuria na kuzungumza moja kwa moja na watu wanaokuja kutazama filamu hiyo ili wamueleze mtazamo wao na ushauri wao kwa ujumla.

Filamu ya Going Bongo, ina mkasa/simulizi la kuvutia na cha kusisimua linalomhusu daktari, Lewis Buger ambaye alijitolea kutoka Los Angeles Marekani kuja Tanzania kufanya kazi kwa muda wa wiki moja.

Hata hivyo, safari yake ilijaa visa na changamoto kubwa za maisha ya Tanzania tofauti ya alivyokuwa amezoea Marekani.

Akiwa Tanzania, Dk. Burger anakutana na changamoto ya kuishi katika nyumba ambayo ilikabiliwa na tatizo la mgao wa umeme muda wote huku akipambana na joto kali, mbu na mazingira duni ya maisha.

Dk. Burger pia alikutana na changamoto kubwa katika hospitali aliyokuwa akiifanyia kazi ambapo pamoja na kukabiliwa na mgao wa umeme, jenereta la hospitali lilikuwa bovu huku idadi kubwa ya wagonjwa ikiwazidi madaktari.

Akiwa daktari aliyejikita katika upasuaji, wakati mwingine alilazimika kufanya zoezi la upasuaji bila kuwa na umeme.

Dk. Burger akiwa Uswahilini

Dk. Burger akiwa Uswahilini

Baadhi ya wagonjwa wake walikuwa wanaamini ushirikina zaidi na kukataa dawa za hospitali, hali iliyomfanya wakati mwingine kujifanya mganga wa kienyeji ili awatibu wagonjwa aliokuwa anawapenda. Hata hivyo aliumbuka kupitia mpango huo.

Dk. Burger pia alikuwa na mpenzi wake mtoto wa tajiri nchini Marekani ambaye alikuwa na drama ya aina yake huku akikutana na mrembo mwingine wa kizungu nchini Tanzania aliyefanya naye kazi.

Mrembo aliyeigiza kama Mchumba wa Dk. Burger

Mrembo aliyeigiza kama Mchumba wa Dk. Burger

Mitego, wivu, vituvo, lugha gongana, huzuni na drama viliwafanya watazamani mara kwa mara kuangua vicheko na wakati mwingine kusononeka.

Ni Arsenal Vs Barcelona Hatua Ya 16 Bora
Vanessa, Ali Kiba washinda Tuzo Za Nzumari za Kenya