Gugu karoti ambalo kwa kitaalamu linajulikana kwa jina la (Parthenium hysterophorus), limegeuka tishio kwenye eneo la Terati ambalo ni nyanda za malisho kwa wanayama pori na wanyama wafugwao mkoani Arusha kwa kusabibisha vifo vya wanyama hao.

Imeelezwa kuwa licha ya mifugo kufa, wananchi wanaposhika majani hayo wanapatwa na upele, ng’ombe wanapokamuliwa maziwa yake yanakuwa machungu na kuwasababishia muwasho mkali.

Wananchi wa kijiji hicho wameiambia Uhuru kuwa wanaomba serikali ichukue hatua za haraka ili kunusuru mifugo yao kwani magugu hayo yameenea maeneo mengi ya mkoa wa Arusha.

Loishiye Mollel amesema wafugaji wanapata hofu ya mifugo yao kufa kutokana na gugu karoti kuchanganyika kwenye majani ya kawaida waliyozoea kulisha mifugo hivyo ni rahisi kula na kupoteza maisha.

“Tunaiomba serikali itusaidie kupata dawa ya kuteketeza gugu hili hatari ambalo linaathiri mifugo yetu na wakati mwingine inapoteza maisha kwasababu mpaka sasa hatujajua dawa ya kutibu mifugo inayokula gugu hili ambalo linasambaa kwa kasi kila sehemu na kuzuia majani ya aina nyingine kuota” amesema Mollel.

Paulina Saningo amesema awali walipoona gugu hilo ambalo linachanua maua meupe walidhani ni jani la kawaida na walipokata na kupelekea mifugo ghafla maziwa yaliyokamuliwa yakawa machungu na waliokata majani hayo walianza kupata miwasho mikali na vipele mithiri ya mgonjwa wa ukurutu.

Na ameongeza kuwa ” Ukinywa maziwa unapatwa na muwasho mkali na kuanza kutoka vipele ambavyo vinawasha sana hali ambayo imeathiri watu wengi, pia watoto wetu wanakosa lishe bora kwa kukosa maziwa ambayo ni muhimu”.

Mtaalamu wa kilimo na mifugo wa kujitolea Charles Bonaventure amesema gugu hilo linaweza kudhuru au kuuwa wanyama lisipodhibitiwa kutokana na kuwavimbisha matumbo kunakosababishwa na kemikali inayofahamika kwa jina la ”alkaloid” ambayo huwa inaua bakteria wanaosaidia wanyama kwenye mmeng’enyo wa chakula.

Bonaventure  amesema jani hilo linaloenea kwa kasi lina uwezekano wa kuingia kwenye hifadhi ya taifa ya Tarangire kutokanana na asili yake ya kuenea kwa kasi na huenda likaathiri vivutio vya utalii.

“Mmea huu unapokomaa hutoa mbegu kati ya 25,000 na 30,000 ambazo husafirishwa na maji kuelekea kwenye maeneo mbalimbali amabyo hayajafikiwa na hudumaza mimea mingine salama kwa malisho ya wanyama kwa kupumua sumu kupitia kwenye mizizi inayofahamika kitaalamu kama ”allelopathic” baaada ya kudhuru hutawala eneo lote la ardhi na kubaki lenyewe”  alisema mtaalmu huyo.

Barani Afrika gugu hilo vamizi limeonekana kuleta athari katika nchi za Afrika Kusini, Ethiopia na kusambaa kwa kasi Uganda,Kenya na hatimaye Tanzania.

Tanzania utafiti unaonyesha gugu karoti kwa mara ya kwanza lilionekana mkoani Arusha mwaka 2010  kwenye barabara kuu ya Arusha-Moshi na uwanja wa ndege Arusha.

DC Tunduru apiga marufuku sherehe za wazazi kwa wanaohitimu darasa la saba
Polisi kuwasaka wanaotaka kujinyonga Tabora