Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini – LATRA, imetakiwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika sekta ya usafirishaji ili kuimarisha mahusiano katika sekta hiyo na kusema Binadamu yeyote anataka asikilizwe hivyo kutaka uwepo wa vikao vya mara kwa mara na kusikiliza changamoto mbalimbali.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa wakati akizindua bodi mpya ya mamlaka hiyo na kuainisha sababu ya changamoto zinazojitokeza katika sekta hiyo pamoja na kuweka bayana njia za kutatua changamoto hizo.

“Binadamu yeyote anataka asikilizwe kwahiyo ninaomba sana bodi hii muwe na vikao vya mara kwa mara na hawa wadau mfano wamiliki wa mabasi, kaeni nao muwasikilize changamoto zao, wakati mwingine inatokea hata migomo lakini mngekuwa mnakaa mnaweza kufanya haya yasitokee,” amesema Mbarawa.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa.

Mbarawa amesema, “Hakikisheni mnashughulikia malalamiko ya wafanyakazi, na wadau pamoja na kuboresha huduma kwa wateja, Wapeni fursa wakajionee, leo mtu anashughulika na Tazara lakini hapajui wala hajui uendeshaji wake, wapelekeni wakaone itasaidia wao kufanya kazi kwa ufasaha zaidi.”

Aidha ameongeza kuwa, “Fanyeni uchambuzi wenye uhakika alafu mje mtu shauri, ninaamini mkifanya hivyo mtaasaidia sana hata kupunguza ajali za barabarani, mkishafanya uchambuzi wenu njooni na suluhisho la nini kifanyike mtakuwa mmesaidia pakubwa.”

Kwa upande wao, Mkurugenzi mkuu wa LATRA, CPA. Habibu Suluo pamoja na Mwenyekiti mpya wa Bodi hiyo Prof. Ahmed Mohamed Ame wamesema lengo lao ni kuendelea kufanya kazi kwa ubora, ili kuipa hadhi mamlaka hiyo.

Donny van de Beek kusepa Man Utd
Kocha Bares aahidi mazito Mashujaa FC