Serikali nchini, imewaagiza wakurugenzi wa Halmashauri kutoidhinisha maombi ya kuhama yanayowasilishwa na watumishi wapya ambao wanaopangiwa vituo vyao vya kazi katika maeneo mbalimbali.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-TAMISEMI), Deogratius Ndejembi Bungeni jijini Dodoma na kuongeza kuwa mtumishi anapaswa adumu katika kituo cha kazi alichopangiwa kwa angalau miaka mitatu mara baada ya kupata ajira.
Amesema, “Mtumishi anapopangiwa kituo chake cha kazi hapaswi kuhama hasa katika kipindi cha matazamio, nawaagiza wakurugenzi kutoidhinisha maombi hayo ya kuhama chini ya muda huo.”
Agizo hilo, lilitolewa baada ya wabunge wa majimbo ya Mchinga la Salma Kikwete na lile la Liwale linaloongozwa na Zuber Kuchauka kuitaka Serikali kueleza mkakati wa kudhibiti watumishi wa afya wanaopangiwa kwenye Halmashauri, lakini huondoka.