Mabingwa wa soka Tanzania bara, Young Africans watamkosa kiungo wao Haruna Niyonzima kwenye mchezo wa kwanza wa ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly utaochezwa tarehe 9 mwezi ujao jijini Dar.

Kiungo huyo kutoka nchini Rwanda, ataukosa mchezo huo wa raundi ya mwisho ya kufuzu hatua Nane Bora kufuatia kuoneshwa kadi mbili za njano katika mechi mbili dhidi ya APR ambapo Yanga walifanikiwa kuchomoza na ushindi wa jumla ya mabao 3-2.

Katika mchezo wa awali jijini Kigali, Niyonzima aliyekuwa nahodha alipewa kadi ya njano na hivyo hivyo katika mchezo wa marudiano jijini Dar alioneshwa kadi ya njano mapema kipindi cha kwanza.

Mwaka juzi Niyonzima alikosa pambano la marudiano dhidi ya Al Ahly baada ya kuugua malaria, hali hiyo ilijirudia mwaka jana alipokosa pambano la marudiano dhidi ya Etoile du Sahel baada ya kuumia.

Wachezaji wengine wa Yanga, Donald Ngoma na Amissi Tambwe itabidi wacheze kwa tahadhari katika mchezo ujao baada ya kuonyeshwa kadi za njano.

Majaliwa aeleza siri ya Magufuli kuteua Wakuu wa Mikoa Majenerali wa Jeshi
Azam FC Kupambana Na Esperance Sportive de Tunis