Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameeleza sababu zilizopelekea Rais John Magufuli kuteua Majenerali wa Jeshi wastaafu kuwa wakuu wa Mikoa katika baadhi ya mikoa.

Akiongea hivi karibuni Mkoani Kagera, Waziri Mkuu alisema kuwa moja kati ya sababu zilizopelekea Rais Magufuli kumteua Meja Jenerali mstaafu, Salum Mustafa Kijuu kuwa Mkuu mpya wa Mkoa huo, ni kutokana na kukithiri kwa uhalifu unaotokana na uhamiaji haramu mkoani humo.

Alisema kuwa maeneo mengi ya pembezoni mwa nchi yamegeuzwa kuwa maficho ya wahamiaji haramu ambao huwaletea shida kubwa wenyeji baada ya kuanza shughuli zao za uvunjifu wa sheria, hivyo uzoefu wa Jenerali huyo mstaafu wa kikosi cha waenda kwa miguu utakuwa mwarubaini.

“Hapa kwenu Kagera kuna tatizo kubwa la waharamiaji haramu na uvamizi wa ardhi. Wavamizi wengine wanalima bangi katika maeneo yetu badala ya kufuga na kulima. Waondoeni au punguzeni maeneo yao na lindeni mipaka yetu.

“Mapori ya Kimisi na Burigi yamegeuzwa maficho ya wahamiaji haramu, ndio maana tumemleta Meja Jenerali Kijuu. Shughuli yake huyu siyo nyepesi. Atatembea mwenyewe huko. Huyu si alikuwa Kamandi ya Infantry (askari wa miguu), kwa hiyo ataimudu shughuli hii vizuri,” Waziri Mkuu Majaliwa anakaririwa.

Rais Magufuli alifanya uteuzi wa Wakuu wa Mikoa wapya huku taswira ya Wanajeshi Wastaafu zikionekana hususan katika mikoa ambayo imekuwa na usugu wa matukio ya kihalifu na migogoro ya ardhi. Wanajeshi wengine waliotajwa kwenye orodha hiyo ni Meja Jenerali mstaafu, Ezekiel Kyunga (Geita), Meja Jenerali mstaafu, Raphael Muhuga (Katavi) na Brigedia Jenerali mstaafu Emmanuel Maganga (Kigoma).

Mabingwa Wa Afrika Kupambana Na Wydad Casablanca
Haruna Niyonzima Kuwakosa Waarabu Wa Misri