Kwa mujibu wa tafiti zimeeleza kuwa wanawake 300,000 hususani wanaoishi katika nchi zinazoendelea hufariki dunia kila mwaka kutokana na upasuaji.
Utafiti uliofanywa na chuo cha Queen mary jijini London, nchini Uingereza umetoa takwimu za vifo hivyo na ndio utafiti unaoaminika zaidi kuliko tafiti nyingine zilizowahi kufanyika nchini humo.
Ripoti ya tafititi hiyo imeambatanishwa na takwimu za wanawake wajawazito milioni 12 na wakagundua kuwa hatari ya vifo kutokana na upasuaji katika nchi zinazoendelea iko juu kuliko walivyotarajia kabla hawajaanza kufanya tafiti hiyo.
Njia ya upasuaji wakati wa kujifungua imekuwa ikisaidia kuokoa maisha ya Mama na watoto wao, lakini katika maeneo mengi ya kusini mwa jangwa la sahara imegeuka mwiba kwa kusababisha vifo vya wanawake.
Imeelezwa kuwa idadi ya wanawake wanaopoteza maisha katika nchi zinazoendelea ni mara 100 zaidi ya nchi zilizoendelea kama vile Uingereza na asilimia kumi ya watoto wote hufa wakati au baada ya upasuaji.
Utafiti huo uliochapishwa kwenye jarida la masuala ya afya, Lancet umewataka wanawake katika nchi zinzokabiliwa na changamoto hizo kupata huduma nzuri za upasuaji zenye kutekelezwa na watu walio na utaalamu kuhakikisha kuwa upasuaji unafanyika kwa usalama wa hali ya juu.