Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye ameibuka na kuwatetea wakulima baada ya serikali kutangaza hivi karibuni kuanza kutowalipa pesa wakulima wanaomiliki korosho walizozipata kwa kuzinunua kutoka kwa wenzao kwa mfumo wa ‘kangomba’ pasipo kuwa na mashamba.
Amesema kuwa mfumo huo unaoendelea sasa unawapa mateso wakulima na kupendekeza kuwa ili kumaliza tatizo hilo, ni vyema serikali kuviwezesha vyama vya ushirika kupitia Benki ya Maendeleo ya Wakulima (TADB) kulipa sehemu ya malipo kwa wakulima hao mara tu korosho inapofika ghalani.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Nape Nnauye ameandika kuwa, “Dawa ya kangomba ni kubadili mfumo wa malipo ya korosho kwa wakulima, kwa kuviwezesha Vyama vya Ushirika kupitia TADB kulipa sehemu ya malipo mara tu korosho inapofika ghalani, hiki kinachoendelea kwasasa hakiwezi kumaliza kangomba, ni mateso tu kwa wakulima!,” ameongeza Nape.
Aidha, Rais Magufuli wakati akitangaza uamuzi wa serikali kununua korosho za wakulima, Novemba 13 Jijini Dar es salaam alisema kuwa serikali itanunua korosho zote za wakulima kwa bei ya sh. 3,300 kwa kilo baada ya wanunuzi binafsi kushindwa kutimiza matakwa ya serikali.