Kiungo mkabaji wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Himid Mao ‘Ninja’, ataukosa mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Tanzania Prisons keshokutwa (Februari 24) kufuatia kutumikia adhabu ya kukosa mechi moja baada ya kukusanya kadi tatu za njano.

Nahodha Msaidizi huyo wa Azam FC alionyeshwa kadi ya tatu ya njano juzi jijini hapa, wakati walipoichapa Mbeya City mabao 3-0 na sasa ataruhusiwa kucheza katika mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Panone (Februari 28 mwaka huu) au ataweza kukipiga  wakapokipiga na Yanga kwenye ligi (Machi 5, mwaka huu).

Akizungumza na mtandao wa www.azamfc.co.tz Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, amesema kuwa pengo la kiungo huyo litazibwa na Salum Abubakar ‘Sure Boy’, anayerejea dimbani baada ya kumaliza kutumikia adhabu kama hiyo ya Himid walipocheza na Mbeya City.

“Natarajia Sure Boy atarejea na kuziba mahala pa Himid, lengo langu ni kumtumia Sure Boy na nasubiria kuona katika mazoezi ya mwisho kesho,” alisema.

Hall pia alisema huenda akaendelea kumtumia winga Ramadhan Singano ‘Messi’ kucheza namba 10 baada ya kufanya vizuri sana katika mchezo uliopita dhidi ya Mbeya City.

Messi amekuwa na kiwango kizuri sana hivi sasa baada ya kuanza kuzoeana na wenzake na kuushika mfumo wa 3-5-2, unaotumiwa na Azam FC jambo ambalo limemfanya aanze kuaminiwa na kuanza kikosi cha kwanza katika mechi mbalimbali za hivi karibuni.

Wachezaji wengine wa Azam FC watakaoendelea kuikosa mechi hiyo ni mabeki Aggrey Morris, Abdallah Kheri na Racine Diouf  pamoja na mshambuliaji Didier Kavumbagu, waliokuwa majeruhi wakiendelea na maandalizi ya mwisho kurejea uwanjani.

Ushindi wowote wa Azam FC keshokutwa utaifanya kurejea kileleni mwa msimamo wa ligi kwani itafikisha jumla ya pointi 48 na kuizidi pointi mbili Yanga itakayoangukia nafasi ya pili wakiwa na pointi zao 46 huku Simba ikikamata nafasi ya tatu wakikusanyia 45.

Anna Mghwira apaza sauti kuhusu Mgombea urais wa Zanzibar aliyewasaliti
Rais Wa Inter Milan Akanuasha Uvumi Wa Kumuajiri Mourinho