Hivi karibuni katika mitandao ya kijamii kumekua na tuhuma mbalimbali zinazorushwa kwa mbunge wa kuteuliwa Humprey Polepole juu ya swala la rushwa ya pesa na rushwa ya ngono.

Katika Mahojiano Maalumu aliyofanya na Dar24 Media mbunge huyo ndugu Humprey Polepole ametolea ufafanuzi maswala hayo na mwenendo mzima wa Uchaguzi wa mwaka 2020

Kuhusiana na kuomba au kupokea Rushwa ya Ngono Polepole amesema hizo zote ni njia za wasiomtakia mema na waliokua hawamtaki katika safu ya uongozi wa CCM huku akimuhoji mwandishi wa Dar24 Media kama aliomba au alipewa Ngono.

“Kwenye Chama Cha Mapinduzi ukiwa umenyooka kama rula kuna mambo manne ambayo utahusishwa nayo, ambayo ni kupigwa fitna ambapo watapeleka maneno ya uongo kwa viongozi, pili utashushiwa zengwe ambapo utatengenezewa skendo ambayo haina kichwa wala miguu, tatu utarogwa na utakufa hivihivi, Uchawi upo kwa wanasiasa na nne watataka kuumiza kwa kukuvizia” amesema Polepole

“Mimi najivuna namtegemea Mungu hata ibilisi mwenyewe ukimuendea anakukatalia huyo tumuache, mimi niko vizuri huwezi kuniroga kwa mganga wala kunigusa, namtegemea Mungu”

Kuhusiana na swala la Rushwa ya pesa analotuhumiwa nalo Polepole wakati wa kutia nia kipindi cha uchaguzi wa wagombea wa CCM, amesema hakuwahi kuhusika na swala hilo na kama yupo ambae alichukuliwa hela amekiuka kanuni na katiba ya chama

“Na imeandikwa hata kwenye ahadi za mwanachama wa CCM kuwa Rushwa ni adui wa haki, sitatoa wala kupokea rushwa, na kama wewe ulitoa rushwa wewe ni mhalifu, na kama uliombwa rushwa uko utaratibu wa kimaadili wa chama ulitakiwa kutoa taarifa, sijawahi kupata tuhuma ya rushwa na niliwahi kupewa barua ya pongezi kwa kufanya kazi nzuri” Ameongeza Polepole

Humphrey Polepole amesema ili mtu awe mbunge kuna hatua zinazopitia watu wengi ambao ni wajumbe wa chama, kamati zote za chama, usalama na sheria hadi kufika halmashauri kuu na haikua kazi ya mtu mmoja

Polepole katika kuzungumzia mwenendo mzima wa uchaguzi amesema, Uchaguzi mkuu unaendeshwa kwa kwa mujibu wa katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania, sheria ya uchaguzi, na sheria nyingine zote ambazo zinatoa msaada kwa zoezi zima la uchaguzi

“sijasikia kesi inayohusu chaguzi au inayohukumiwa kwamba uchaguzi wa mwaka 2020 haukua huru na haki, mpaka sasaivi kwa mimi nilieshiriki kwa asilimia mia moja ninaamini hapakua na tatizo isipokua tu watu wengi waliotarajia kushinda hawakushinda”

Amesema wapinzani hawakushinda sio kwa sababu kulikua na tatizo katika zoezi zima la uchaguzi bali hawakuwa na sera za kuwavutia wananchi

Polepole ameongeza kuwa kama serikali ingekua haifanyi kazi na mihimili yake kama Bunge na Mahakama ndipo inahalalisha kulikua na tatizo lakini kwa sasa hakuna kesi yoyote inayohusu uchaguzi wa mwaka 2020.

“na mimi rai yangu wabunge wote waliopita katika uchaguzi huo wachape kazi kwa sababu tuna mambo ambayo tuliyafanya mwaka 2015 -2020 wanatakiwa wayaendeleze” alimalizia Polepole

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Disemba 28, 2021
Polepole ataja wahuni wote