Baraza la wazee wa klabu ya Young Africans, limeridhia kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa viongozi wa klabu hiyo kama ilivyotangazwa jana na kamati ya uchaguzi ya shirikisho la soka nchini TFF.

Kauli ya baraza hilo la wazee imetolewa na katibu mkuu wake mzee Ibrahim Akilimali, wakati akizungumza mapema leo na kuwasihi wanachama wapiga kura wa klabu hiyo kongwe nchini kutofanya uchaguzi wa kishabiki na badala yake kuangalia maendeleo ya mbele.

Akilimali amesema Young Africans inahitaji kwenda mbele na kutisha kimataifa katika medani ya soka la kisasa na kusema kuwa yote hayo yanawezekana lakini kwa kuweka madarakani viongozi wenye uwezo wa kuyatimiza hayo kwa vitendo na siyo maneno matupu.

‘Nawasihi wanachama wenzangu waache ushabiki na badala yake wachague viongozi kwa kuangalia maslahi ya klabu na maendeleo yake kwa ujumla’

‘Viongozi wenye uwezo wanafahamika na wala hakuna haja ya kutapa tapa kwenye hilo na kinachotakiwa ni utekelezaji wa kuwaweka madarakani ili tuweze kufikia malengo yetu ya kuwa klabu bora barani afrika’Alisema mzee Akilimali.

Wakati Young Africans ikijiandaa kuingia kwenye mchakato huo wa uchaguzi, maswali mengi yamekuwa yakizunguka katika vichwa vya wanachama na mashabiki kuhusu katiba itakayotumika katika uchaguzi huo, kwani shirikisho la soka nchini TFF ilishaagiza muda mrefu kwa wanachama wake kufanya mabadiliko ya katiba kulingana na wakati.

Kwa sasa Young Africans tangu itangaze kufanya mabadiliko hayo ya katiba na kuyawasilisha TFF, hakuna majibu yeyote yaliyopatikana yakieleza uhalali wa matumizi yake kiasi cha kuwafanya watu wazidi kupigwa na butwaa.

Young Africans inaongozwa na mwenyekiti wake Yusuph Manji ambaye muda wake wa uongozi kikatiba umekwisha tangu mapema mwaka uliopita, baada ya kuongezewa kipindi kingine cha mwaka mmoja kinyume na katiba ya zamani lakini tangu kipindi hicho cha nyongeza kumalizika bado Manji anaendelea kuwepo madarakani bila ya sababu za msingi.

Kutokana na hali hiyo TFF kupitia kamati yake ya uchaguzi chini ya mwenyekiti wake wakili, Aloyce Komba, imetangaza Juni 05, 2016 kuwa siku ya uchaguzi mkuu wa viongozi wa Young Africans.

Imesema mchakato mzima wa uchaguzi wa klabu ya Young Africans utakuwa ndani ya siku 33, na unatarajiwa kuanza rasmi Mei 03, 2016.

Tiboroha: Sina Mpango Wa Kugombea Nafasi Yoyote
Rais Magufuli avunja bodi ya TCRA, Amuondoa Mkurugenzi Mtendaji