Rais John Magufuli leo amevunja Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dk. Ally Simba kwa kushindwa kusimamia mkataba wa utekelezaji wa mfumo wa usimamizi wa Mawasiliano ya simu (TTMS), hivyo kupelekea Taifa kukosa mapato ya takribani shilingi bilioni 400 kwa mwaka.

Dk. Ally Simba

Dk. Ally Simba

Taarifa iliyotolewa leo na Kurugenzi ya Ikulu, imeeleza kuwa Rais Magufuli amechukua hatua hiyo leo alipofanya kikao kazi na viongozi na wataalam kutoka Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Wizara ya fedha na Mipango na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Taarifa hiyo imefafanua kuwa, tarehe 22 Machi, 2013 Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) iliingia mkataba na kampuni ya SGS juu ya uwekaji, uendeshaji na uhamishaji wa mapato ya simu ambapo kampuni hiyo ilipaswa kutekeleza vipengele vitano lakini mpaka sasa kampuni ya SGS haijaanza kutekeleza kipengele kidogo kinachohusiana na uthibiti wa mapato ya simu za ndani (Offnet), hali ambayo imesababisha serikali kukosa mapato yanayokadiriwa kuwa shilingi bilioni 400 kwa mwaka.

Kutokana na hali hiyo, Rais Magufuli amewataka Waziri Prof. Mbarawa, Katibu Mkuu na Naibu Katibu katika wizara hiyo kuchukua hatua mara moja ili mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya simu kwa simu za ndani (Offnet) uanze kufanya kazi, na nchi ipate mapato yanayostahili kukusanywa.

“Waziri hakikisha unachukua hatua mara moja, nataka tukusanye mapato yote ya serikali yanayostahili na sitasita kuchukua hatua dhidi ya yoyote atakayekwamisha jambo hili” Amesisitiza Rais Magufuli.

Ibrahimu Akilimali: Wanachama Msichague Kiongozi Kwa Ushabiki
Taifa Stars Kupambana Na Harambee Stars Mwezi Ujao