Katika hali ya kusikitisha, wapendanao waliokula kiapo cha kuvumiliana kwenye shida na raha, afya na maradhi wamelazimika kukiweka kando kiapo chao na kujikuta wakiwa katika hali ya sintofahamu baada ya kupokea zawadi ya picha chafu za bibi harusi akifanya mapenzi kinyume cha maumbile.

Tukio hilo la kusikitisha limetokea jijini Dar es Salaam hivi karibuni, ambapo kwa mujibu wa maelezo ya wanandoa hao pamoja na rafiki wa mume aliyewasindikiza katika tukio la ndoa (best man), walipokea picha hizo wiki siku moja baada ya kutoka kwenye fungate (honeymoon).

Akizungumza na kipindi cha Ubaoni cha E-Fm hivi karibuni, rafiki wa bwana harusi aliyejitambulisha kwa jina la Geoffrey Nicholaus alisema kuwa yeye ndiye aliyekuwa wa kwanza kuziona picha hizo wakati alipokuwa akifungua zawadi za maharusi hao baada ya kutoka kwenye fungate, Juni 29 mwaka huu.

“Nilikuta ndugu zake wote wako pale. Nikakuta kuna mabox ya zawadi pale kwahiyo akaniomba nimsaidie pale kufungua mizigo ya zawadi. Sasa wakati tunaanza shughuli ya kufungua Box la kwanza… la pili nikaona zile picha, zile picha za mke wake sio nzuri kwakweli nishtuka,” Geoffrey alisema.

“Sasa mimi wakati nataka kuficha ile kitu, yule jamaa akaniona akaniuliza ‘mbona unashtuka bana kuna nini au kuna bomu nini… nikamwambia hamna kitu bana. Akaja akaziona zile picha na yeye akashikwa na butwaa kwa sababu zile picha hata nikikuonesha ni mbaya sana. Jamaa akaanza kupiga makelele pale, akawa kachanganyikiwa” alisema.

Rafiki huyo wa Bwana Harusi alieleza kuwa tangu rafiki yake alipoziona hizo picha akili yake haikuwa sawa na hakutaka kumuelewa mtu yeyote licha kufanyika kwa vikao mbalimbali vya familia. Ameeleza kuwa rafiki yake huyo hahudhurii vikao hivyo lakini pia hapokei simu yoyoe ya upande wa mkewe kwakuwa anaamini walifahamu suala hilo mapema ila hawakutaka kumwambia.

Mwanamke huyo ambaye ndoa yake imegeuka msiba mkubwa moyoni mwake  alikiri kuwa picha hizo ni zake na kwamba alipiga wakati alipokuwa na mpenzi wake wa zamani, miaka mingi iliyopita.

“Nimeumia sana, nimedhalilika sana. Kwakweli picha ni za kwangu, ni picha ambazo ni kweli nilipiga na mpenzi wangu wa zamani. Sio nzuri. na huyo mtu alikuwa mpenzi wangu lakini ilikuwa zamani sana. Mimi mwenyewe hata sielewi,” alisema mwanamke huyo huku akilia.

  Mwanamke huyo alilaani kitendo alichofanyiwa na mpenzi wake huyo wa zamani huku akionekana kutokuwa katika hali nzuri kisaikolojia kufuatia tukio hilo. Kipindi hicho pia kilifanikiwa kumpata mume wa msichana huyo na kufanya naye mazungumzo lakini aliweka msisitizo kuwa hajui cha kufanya zaidi ya kuachana na mkewe. “Sijui nisemeje kwakweli, cha kuzungumza mimi sina. Yaani kilichotokea pale ndio hicho kilionekana. Yaani sikuamini macho yangu, yaani picha ziko vile na yule mwanamke! Pakuanzia sipajui….lakini anyways. Watu wote walikuwa pale, rafiki yangu, ndugu zangu,” alisema kwa uchungu.

“Kama ungekuwa wewe ungekaa chini na yule mwanamke ili iweje. Yaani kusoma hujui lakini hata picha huoni? Sawa hata kama imetokea miaka 10 iliyopita. Bora angekuwa ameniweka wazi lakini alinificha. Kwakweli imeniuma, kwa familia yangu kwa mfano unafikiri mimi nitasema nini? Kamuulize yule mwanamke umuulize ilikuwaje sio mimi kwakweli inaniuma.

Mwanaume huyo alieleza kuwa hataweza kuwa na mwanamke huyo tena huku akila kiapo cha kutokuoa tena hadi maisha yake yatakapofika kikomo.

My Take: Hili ni tukio baya, la kusikitisha sana. Kosa alilofanya mwanamke huyo kutokana na upofu wa mapenzi ulioziba ufahamu na utashi wake limegeuka mwiba mkuu moyoni mwake. Lakini huu sio muda wa kumlaumu bali wote wawili wanapaswa kusaidiwa kisaikolojia ili maisha yaendelee.

Vyombo vya dola vinapaswa kuchukua hatua kali za kisheria juu ya tukio hilo kwani aliyetuma zawadi hiyo tayari amefahamika na picha hizo zinamuonesha.

 

Diego Costa Akanusha Kuondoka Chelsea
Juventus Kumsajili Marko Pjaca