Mtu anapojitambulisha kuwa anafanya kazi mgodini, watu wengi hudhani kuwa kazi zilizopo ni kuingia chini ya ardhi kutafuta madini pekee, dhana hiyo imesababisha baadhi ya watu kuamini kuwa kazi yoyote mgodini ni ya wanaume, lakini dhana hiyo ni tofauti kwa Neema Mwidibo ambaye amefanya kazi katika sekta ya madini kwa miaka 20 sasa.
Mwidibo ambaye sasa ni mama wa watoto wanne, alihamia katika Kampuni ya Geita Gold Mining Limited mwaka 2005 na kuanza kufanya kazi kama mpokezi wa taarifa kupitia redio na kuingiza data akiwa na elimu ya kidato cha sita pekee.
Hivi sasa mama huyu ni Afisa Mwandamizi katika idara ya manunuzi anaelezea historia yake mpaka kufikia mafanikio hayo akisema, “nilizaliwa katika Kijiji cha Nyarugusu kilichopo Geita Mjini, baada ya kumaliza elimu ya kidato cha sita mkoani Geita, nilipata hamasa ya kufanya kazi mgodini baada ya kuona ndugu zangu walioajiriwa na Kampuni ya GGML wakifanikiwa kimaendeleo.”
Katika mazungumzo yake na mwandishi wa makala haya, anasema alipojaribu kutuma maombi ya kazi ndani ya mgodi, alipata kazi kwa mkandarasi mmoja aliyekuwa amepewa zabuni na GGML, kisha baada ya miaka miwili ndipo akahamia GGML kama mpokezi wa taarifa kwa njia ya redio na mhifadhi data.
Kwa kuwa elimu yake ilikuwa ndogo, alipata hamasa ya kujiendeleza kielimu hivyo akawa anaweka akiba ya fedha ili kutimiza lengo hilo na alijiunga na masomo ya masafa marefu katika chuo cha Cambridge nchini Uingereza na kufanikiwa kupata Stashahada ya manunuzi ambayo sasa ilimuwezesha kuhamia katika idara ya manunuzi ndani ya GGML.
Anasema baada ya mwaka mmoja na ushee, aliamua tena kurudi chuo na kujiunga na masomo ya Shahada ya masuala ya manunuzi (Bachelor of Arts in Procurement and Supply Chain Management) ambapo ilimbidi aache kazi ili aweze kupata muda wa kutosha katika masomo yake ambapo baada ya kumaliza masomo, alirejea GGML akapokelewa na kupatiwa nafasi ya juu zaidi kama Afisa manunuzi mwandamizi kwenye kitengo hicho cha manunuzi.
MCHANGO WA GGML
Anasema hii inaonesha ni kwa namna gani kampuni ya GGML imekuwa na mchango wa kipekee katika maisha yake hadi kufanikiwa kukua kitaaluma na kuongeza kuwa, “kwa sababu wote tunafahamu umuhimu wa ajira, kuwa muajiriwa imenisaidia kuendesha maisha yangu. Ninaweza kuhudumia familia na kufanya biashara mbalimbali.”
Anatolea mfano kuwa hivi karibuni alipatiwa mafunzo maalumu ya kuwajenga wanawake kushika nyadhifa za juu za uongozi (Female Future Tanzania Program – FFT) ambayo yalimsaidia kupiga hatua hadi kushika wadhifa wa Afisa mwandamizi ndani ya kampuni hiyo.
“Katika mafunzo hayo nilikutana na wanawake wenye nafasi kubwa kwenye makampuni tofauti tofauti, hali hiyo ilinifanya niamini kwamba inawezekana na mimi kama mwanamke kufikia ngazi za juu. Nikiwa katika mafunzo yale nilijifunza mambo mbalimbali ya uongozi na program nyingine tofauti tofauti,” anasema.
Anasema ndani ya GGML, wanawake wanapewa kipaumbele kikubwa katika fursa mbalimbali kuanzia, mafunzo ndani ya kampuni, elimu na hata ajira na kwamba “ninawapa hamasa wanawake wenzangu kushiriki mafunzo mbalimbali na kujiendeleza kielimu kwa sababu hapa nilipo ni kwa sababu ya sekta ya madini, kwanza mazingira ya kazi ni salama kwao na kwa maisha yao ya baadae. Mtu akija hapa GGML anaweza kukua kielimu na kikazi vile vile,” anasema.
LINA SITTA
Kauli hiyo ya Neema Mwidibo inaungwa mkono na Lina Sitta – Afisa mwandamizi wa masuala ya mafunzo kwenye idara ya uchenjuaji dhahabu (process plant) katika mgodi wa GGML ambapo safari yake aliianza mwaka 2003 akiwa mwalimu msaidizi katika shule ya watoto ya International School of Geita inayomilikiwa na GGML ambako alifanya kwa muda wa miaka saba kisha akahamishiwa upande wa shule ya msingi ambako alifanya kwa miaka minne.
Baadae alipandishwa cheo na kuwa Afisa usalama na mafunzo ambako alifanya kwa miaka minne kisha baadaye akawa Afisa mwandamizi usalama na mafunzo akisema mafanikio hayo ameyapata kutokana na fursa anazopewa ndani ya GGML kutoka nafasi moja kwenda nyingine na kudai “mafanikio yalikuja hasa kwa kufanya kazi kwa bidii. Mimi ni mwalimu lakini nilitumia zile faida nilizonazo wakaona ninaweza kupanda na kufanya kazi yenye matunda kwa kampuni,” anasema.
Anasema tangu akiwa mdogo aliipenda kazi ya ualimu, ingawa pia alipenda uandishi wa habari na utangazaji na GGML imekuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi za wanawake kwa kuanzisha program mbalimbli ambazo zinaweza kuwainua na kuwaendeleza ili wazitambue haki zao.
“Tumekuwa na program nyingi ikiwamo FFT kwa sababu kila mwaka kuna wanawake wanne au watano wanahitimu mafunzo hayo yanayowaandaa kushika nafasi za juu za uongozi na hata wajumbe wa bodi,” anasema Lina ambaye pia ni mwenyekiti msaidizi wa kikundi cha Geita Ladies ambacho ni mahsusi ndani ya GGML katika kujadili, kushauri na kutatua changamoto mbalimbali za wanawake wanaofanya kazi mgodini hapo, anasema sera za kampuni hiyo zinambeba vyema mwanamke yeyote.
SIKU YA WANAWAKE
Akizungumzia siku ya wanawake duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka Machi 8, Lina anatoa wito kwa jamii kumuandaa mtoto wa kike kuanzia ngazi ya familia ili awe na ujasiri, kujitambua na kujiamini kuwa anaweza kuwa kiongozi, anasema “ni muhimu kuwaandaa watoto wa kike. Majukumu yao sio kuosha vyombo, kubeba mimba na kujifungua, kuna mengine zaidi. Lakini pia jamii inatakiwa kutengeneza ushirikiano ili mtu aendane na mazingira ambayo yatamfikisha mbali zaidi kimaisha.
“Lakini pia kampuni zenye wafanyakazi wa kike ziweke, program mahsusi ambazo zitafanyiwa tathmini kila mara kwamba inapiga hatua kwa kiasi gani kusaidia wanawake hao kukua,”huku akitoa wito kwa wanawake wa GGML na Tanzania nzima kwamba wajitokeze kwa wingi katika nafasi ambazo zinajitokeza hapa GGML, waombe na kuingia kwenye usaili, wakipata nafasi wafanye kazi kwa bidii.
Naye Dkt. Subira Joseph ambaye amefanya kazi GGML kwa zaidi ya miaka 10, anasema kampuni hiyo imempa fursa mbalimbali za kukua kielimu na kitaaluma kwani mwaka 2021 alifanikiwa pia kujiunga na program ya FFT ambayo imemsaidia kujiamini zaidi na kuongeza kwamba,”ninaweza kukabiliana na majukumu mbalimbali kama vile kuongoza idara yangu, ni dhahiri kuwa kupata mafunzo yale yamenisaidia sana,” anasema.
Anasema wakati anaingia GGML hapakuwapo na madaktari wa kike hivyo baadhi ya wafanyakazi wanawake walipata shida kwenda kujieleza kwa madaktari wa kiume ili kupata matibabu hivyo uwepo wa mchanganyiko wa wafanyakazi wanawake na wa kiume umeongeza ufanisi ndani ya kampuni hiyo.
“Ushauri wangu kwa wanawake wengine ni kwamba tusiogope kujiunga na sekta hii ya madini kwani ni sekta kama zilivyo sekta nyingine, hivyo kunapotokea fursa ya kazi tuombe na kuja kufanya kazi kwani hakuna chochote cha ajabu na sekta nyingine,” anasema.
Aidha, Josephine Kimambo ambaye aliajiriwa GGML baada ya kupata mafunzo kwa vitendo alipohitimu masomo ya chuo kikuu, anasema kilichomvutia kufanya kazi kwenye sekta ya madini, kwanza ni sehemu ambayo unajifunza mambo mengi ndani ya kipindi kifupi, ambapo alikuwa mmoja wa wanafunzi 12 waliohitimu program maalumu ya GRP iliyowasaidia kupata mafunzo kazini na kati yao saba walibaki GGML.
“Hivyo ninawahamasisha wanawake wenzangu kuja kwenye sekta hii kwa kuwa sio sekta ngumu. Ndani ya mgodi zipo kada mbalimbali, wanasheria wapo, wahandisi tupo ni maeneo rafiki na mtu anaweza kujifunza, ni tofauti na kampuni ambayo inatoa fursa kwenye eneo moja lakini hapa kuna kila kitu na watu wengi wanatoka maeneo tofauti na mabara mbalimbali,” anasema.
Josephine ambaye ni mhandisi wa mazingira alihitimu Chuo Kikuu cha Ardhi na kupitia programu ya hiyo GRP, mwaka 2012 aliajiriwa GGML na baada ya miaka nane akawa mhandisi mwandamizi katika idara ya mazingira nafasi anayoitumikia hadi sasa.
“Nashauri wanawake wenzangu tuondoe dhana ya upendeleo tuonekane kwa kazi badala ya kuhurumiwa, ninaamini katika utendaji kazi wetu ni chachu hata kwa uongozi kuona kwamba nafasi ikitangazwa nastahili kuomba. Ule uthubutu wa kuomba maana yake una kitu cha kuonesha kutoka ndani yako,” kauli ambayo inaungwa mkono na Melxedeck Mulokozi ambaye ni mrakibu wa usalama katika idara ya usalama kazini, kwenye shughuli za mgodi chini ya ardhi.
Mulokozi ambaye amefanya kazi GGML kwa zaidi ya miaka 14, anatoa ushauri kwa wanawake kwamba watambue wana uwezo wa kufanya jambo lolote tena ikiwezekana kwa ubora zaidi kama ilivyo sasa ambapo Taifa linaongozwa na Rais mwanamke.