Wakati Wakuu wa Mikoa na Wilaya wakihaha kuhamasisha wazazi wawapeleke watoto wao shule kujiunga na kidato cha kwanza, Shule ya sekondari ya Wasichana Nyankumbu imezidiwa kwa wingi wa maombi ya wazazi kuwapeleka watoto wao kutokana na ufaulu na mazingira mazuri ya kujifunzia.

Akiongea na mwandishi wa Habari hii, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Georgia Mugashe amesema katika mwaka huu wa masomo imesajili wanafunzi wapya wa kidato cha kwanza 240 huku ikishindwa kuchukua wengine kutokana na wingi wa maombi.

Amesema, shule hiyo yenye wanafunzi zaidi ya 1,050 imekuwa mkombozi kwa jamii ya wanaGeita kutokana na mwenendo mzuri wa matokeo ya shule katika mitihani ya kidato cha nne sambamba na mazingira mazuri ya kusomea ikiwamo miundombinu bora iliyojengwa na GGML.

Wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Nyankumbu, wakiwa maktaba katika Shule hiyo ya wasichana ya mfumo wa Sayansi yenye Wanafunzi zaidi ya 1050, ikisheheni vifaa vya maabara, nyumba za kisasa 36 kwa ajili ya walimu, madarasa 21 na viwanja vya michezo.

“Wanafunzi 38 walipata daraja la kwanza, 86, daraja la pili, 36 daraja la tatu na sita daraja la nne. Kwa hiyo unaona tunavyopambana kuhakikisha wote wanapata daraja la kwanza kwa sababu hata katika matokeo ya mwaka 2021, waliopata daraja la kwanza walikuwa 50,” alisema.

Aidha, ameongeza kuwa, kutokana na mwamko huo, idadi ya wanafunzi imeongezeka hadi shule kuzidiwa kwani mabweni yaliyopo sasa hayatoshi na kuwaomba wadau pamoja na watu wengine kujitokeza kuendelea kuunga mkono Serikali na GGML katika kuboresha mazingira ya shule hiyo.

Akizungumzia matokeo hayo, Makamu Rais wa AngloGold Ashanti anayesimamia miradi endelevu kwa upande wa Ghana na Tanzania, Simon Shayo alisema inafurahisha na kutia moyo kuona shule ambayo GGML imeianzisha kwa lengo la kuboresha elimu mkoani Geita ikifanya vizuri na kuwa kivutio kwa wazazi.

“Jumla kwenye shule hizi mbili tulitumia Sh milioni 287.5 na kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mji wa Geita, fedha hizi zilitolewa kupitia mfuko huo wa wajibu wa kampuni kwa jamii (CSR),” alisema.

Ameongeza kuwa, “GGML imekuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi za Serikali kwani pia imejenga miundombinu katika shule za Bugando na Kamena ambazo zimeanza kupokea wanafunzi wa kidato cha tano na sita kuanzia mwaka 2021/2022.”

Naye Mwenyekiti wa bodi ya shule kwa upande wa wazazi, Eliangikaya Mshana aliishukuru GGML kwa kuendelea kuungana na wazazi pamoja na jamii ya Geita kuboresha mazingira ya elimu mkoani humo hadi kuwezesha shule hiyo kuwa moja ya shule ya mfano katika mkoa wa Geita.

Shule hiyo ya Serikali, ilijengwa na kuzinduliwa mwaka 2014 na Kampuni ya Geita Gold Miningi (GGLM), kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mji wa Geita kwa kupitia fedha za mfuko wa uwajibika wa kampuni kwa jamii, imetajwa kuwa mkombozi kwa wanafunzi wa kike katika mkoa huo.

GGML ilitumia jumla ya Sh bilioni 15 katika ujenzi wa shule hiyo ya bweni pamoja na kuboresha miundombinu ya shule nyingine za mkoa huo ikiwamo kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuborsha sekta ya elimu nchini.

Leo ni siku ya Redio Duniani
2023: Mwaka wa harakati za kisiasa barani Afrika