Serikali nchini, inaendeleza jitihada za kuzuia na kudhibiti ugonjwa wa shinikizo la juu la damu na magonjwa yasiyoambukiza huku takwimu za mfumo wa ukusanyaji taarifa (DHIS2), zikionesha jumla ya wagonjwa 2,535,281 walitibiwa magonjwa yasiyoambukizwa kwenye vituo vya Afya kwa mwaka 2017.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu hii leo Mei 17, 2023 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya siku ya shinikizo la damu Duniani.
Amesema, “Wagonjwa hawa wameongezeka hadi kufikia wagonjwa 3,440,708 kwa mwaka 2021 ongezeko hili (la wako 905,427 kwa kipindi cha miaka mitano, ni sawa na ongezeko la asilimia 9.4.”
Waziri Ummy amesema kati yao, ugonjwa wa shinikizo la juu la damu ndio uliongoza miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza ambapo waliongezeka kutoka wagonjwa 688,901 kwa mwaka 2017, hadi kufikia wagonjwa 1,345,847 kwa mwaka 2021 sawa na ongezeko la asilimia 95.4 kwa kipindi hicho.
Aidha, ameongeza kwa kusema kuwa wagonjwa waliotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete – JKCI, tangu ilipoanzishwa Septemba 2015 hadi Aprili 2023 kati ya wagonjwa 619,102 tuliowatibu asilimia 66 ya wagonjwa walikuwa na tatizo la ugonjwa wa shinikizo la juu la damu.
Amesema katika uchunguzi uliofanywa katika jamii kwenye mikoa ya Pwani, Arusha, Geita, Mtwara, Lindi, Zanzibar, Iringa na Dar es Salaam takwimu zinaonyesha watu 3-4 kati ya 10 wana shinikizo la juu la damu.
“Shinikizo la juu la damu ndio sababu kubwa (vihatarishi) vya kiharusi (stroke), shambulio la moyo (Heart attack), moyo kushindwa kufanya kazi (Heart Failure), kutuna kwa kuta za mishipa ya damu, moyo, uharibifu kwenye chujio za figo, ganzi miguuni na mikononi, upofu na kupunguza nguvu za kiume,” Amesema Ummy.
Shinikizo la juu la damu ni ugonjwa unaosababishwa na nguvu ya msukumo wa damu katika mishipa kuwa kubwa kuliko kawaida kwa muda mrefu na ongezeko hilo huulazimu moyo kufanya kazi kupita kiasi ili uweze kusukuma damu katika mishipa kwa kiwango kilekile kinachohitajika mwilini.
Kila mwaka ifikapo Mei 17 Dunia huadhimisha siku ya Shinikizo la Juu la Damu ambapo mwaka huu kauli mbiu inasema “Pima Shinikizo la Damu Kwa Usahihi, Idhibiti, Ishi kwa Muda Mrefu” inayolenga kuongeza utambuzi sahihi wa shinikizo la damu ulimwenguni kote, haswa katika nchi zenye kipato cha kati na cha chini ili kuwahamasisha wananchi kujitokeza kupima shinikizo la damu mapema.