Wangoni ni moja ya kabila linalopatikana nchini Tanzania na baadhi ya maeneo mengine kusini mwa bara la Afrika. Ni kabila ambalo lina historia ya aina yake kama ilivyo kwa makabila mengine ya kibantu hata yale yasiokuwa ya kibantu.

Chimbuko la Wangoni.

Kwa mujibu wa maandiko ya Fr. Elzear na Ndugu Romanus Mkinga na masimulizi ya wazee wanasimulia kuwa, Historia na ya asili ya jina la Wangoni linaanzia kusini mwa Afrika. Hapo awali hata kabla ya miaka ya 1000 iliopita, kulikuwa na wakazi wengi wa mwanzo kutoka katika koo za Wazulu waliofahamika kwa jina la Abanguni yaani kwa kiswahili tunaweza kusema Wanguni.

Kwa kipindi chote hiko kwenye ardhi ya kusini mwa Afrika wakazi wote walikuwa wakifahamika kwa jina moja la Wanguni isipokuwa wale Khoisani.

Na kwa miaka yote hiyo walikuwa wakiishi sehemu moja tu na hakukuwa na uhamiaji wowote nje ya ardhi ya Wanguni. Lakini miaka ya 1550, kunaingia wageni kusini mwa Afrika yaani Wadachi. Na ilipofikia miaka ya 1600, kukaja wageni wengine ambao ni Waingereza.

Na kutokana na maslai ya kiuchumi, kidini na kisiasa kulipekea wageni hao kupigana kitu kilichopelekea migogoro mikubwa kusini mwa Afrika, ambayo kimsingi iliathiri sana jamii za Kiafrika Wanguni wakiwemo.

Inasimuliwa kuwa, migogoro hiyo ilipelekea vita vya Mfekane miaka ya mwanzo ya 1800. Na vita hivyo vikasababisha baadhi ya Koo za Kinguni zilizokuwa kwenye makundi makubwa kuhama na kuelekea Afrika mashariki na kati.

Sasa wakati Koo hizo zinatoka huko zilikuwa zikifahamika kama Wanguni. Lakini mambo yalikuja kubadirika kadri sehemu walizokuwa wanapita. Kwa mfano wakati Zwangendaba na Zwinde wanafika kwenye ardhi ya Wathonga waliopatikana maeneo ya Swazland, Wathonga waliwaita Wangoni badala ya Wanguni.

Wao walitoa “U” na kuweka “O” kulingana na sheria na utaratibu wa lugha yao. Na hapo ndipo mabadiliko yalivyoanza kutokea katika zile koo maarufu za Wangoni, kutoka Wanguni hadi kuwa Wangoni.

Wangoni walifanikiwa kufika mpaka Malawi kwenye miaka ya 1840/1850, hapo Malawi kulikuwa na makabila mengi sana. Ila yaliokuwa yakifahamika sanakutokana na biashara ni Wayao ambao nao walikuwa wahamiaji waliokimbia adha ya biashara ya utumwa iliokuwa ikifanywa na Wamakua huko Msumbiji.

Hivyo kwa Wayao, Wangoni waliitwa Wagwangwala wakiwa na maana ya watu wenye haraka, na hii ni kutokana na muonekano wa Wangoni kwenye ardhi ya Wayao, wakiwa wanatembea kwa haraka kuelekea maeneo mengine. Hivyo basi katika ardhi ya wayao huko mashariki ya Malawi tunapata kufahamu kuwa, hapa Wangoni walijulikana kama Wagwagwala yaani watembea kwa Haraka.

Mpaka kufikia kwenye miaka ya 1860, Wangoni walifika kwenye ardhi ya Wahehe. Lakini kabla ya kufika kwa Wahehe, Wangoni walishafika maeneo ya Wasangu na Wabena. Lakini kutokana na kabila la Wahehe kuwa na ulinzi mkubwa na pia kuwa na jeshi imara lenye uzalendo wa hali ya juu.

Hawakuwa tayari kuona ardhi yao ikivamiwa na kukaliwa na wageni ambao hawajulikani walipotoka. Na mwisho wa siku Wahehe waliamua kupigana na Wangoni na kuwatimua katika ardhi ya Uhehe. Na mara baada ya vita hii Wahehe waliwapa jina Wangoni na kuwaita Wamapoma au Wapoma wakiwa na maana ya Wavamizi walovamia ardhi ya Wahehe na kuanzisha mapigano kuanzia kwa Wabena pamoja na Wasangu.

Na mpaka kufikia miaka ya 1870, Wangoni waliweza kufika kwenye ardhi ya Unyamwezi na Usukuma ambapo huko waliitwa Watuta. Na kuna baadhi ya maeneo ya ziwa Tanganyika, Wangoni waliitwa Watuta pia kwa makabila kama Wafipa waliokuwa na ufalme wao kwa wakati huo.

Kwa ujumla tukianza kuuliza kila kabila lililokuwa limefikiwa na Wangoni, tunaweza kupata majina mengi sana kulingana na idadi ya makabila tulionayo. Kwa sababu ujinaishaji wa majina ya makabila yetu ulikuwa unategemea sana mitazamo aidha ya wazawa au wageni.

Tukimaanisha kuwa kuna makabila yamepata majina kutokana na wao wenyewe kujiita hivyo, na kuna wengine walipata majina kutokana na utani au mtazamo wa wageni. Hivyo tunaweza kuwaita Wangoni kwa majina mengi sana lakini urithi wa makabila unategemea masimulizi ya wazee kutoka kizazi hadi kizazi.

Hivyo kama leo hii tunawafahamu Wangoni kama Wangoni, basi hayo ni matunda ya kuhifadhi urithi wa kabila hili. Kama si hivyo pengine wanahistoria wangewajua Wangoni kama Wagwangwala au Watuta.

Kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Ruvuma- CCM, Eng. Stella Manyanya

Jitihada udhibiti magonjwa yasiyoambukiza zinaendelea
Wawili waongezwa kinyang'anyiro Spurs