Meneja wa klabu ya Man Utd Jose Mourinho amesisitiza kufanya usajili wa mchezaji mmoja kabla ya kufunga biashara ya usajili katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi.

Mourinho alizungumza na BT Sport mara baada ya mchezo maalum kati ya kikosi chake dhidi ya Everton kwa ajili ya Wayne Rooney, na kueleza mipango ya usajili wa mchezaji mmoja aliyonayo kwa sasa.

“Tutafanya usajili wa mchezaji mwingine mmoja,” alisema meneja huyo mwenye umri wa miaka 53.

Hata hivyo Mourinho ameshindwa kuthibitisha jina la mchezaji ambaye wanamlanga kwa sasa, na hata alipoulizwa kuhusu kiungo kutoka nchini Ufaransa Paul Pogba ambaye amekua akitajwa kurejea klabuni hapo, hakuwa tayari kuweka wazi.

“Sitaki kuzungumzia suala la Paul, kwa sababu ni mchezaji wa Juventus na mimi sipendi mameneja wengine kuwazungumzia wachezaji wangu. Lakini ukweli ni kwamba tutafanya usajili wa mchezaji mmoja kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili Agosti 31.”

Kwa sasa Man Utd wapo katika harakati za kutaka kukamilisha dili la usajili wa Pogba, na mara kadhaa wamekua wakitaka mpango huo ukamilishwe mapema ili mchezaji huyo aweze kuwa sehemu ya kikosi kitakachocheza michezo ya mwanzo ya ligi ya nchini England.

Lakini pamekua na taarifa za kuwakatisha tamaa mashetani hao kuhusu Pogba, kutokana na klabu ya Real Madrid kuwa katika mkakati wa kutaka kingilia kati na kumuhamishia Estadio Santiago Bernabeu.

Wafugaji wakubwa watakiwa kujiandaa kwa ufugaji wa kisasa
VfL Wolfsburg Wakata Ngebe Za Julian Draxler