Siku moja baada ya kutimuliwa na Chelsea, Kocha mwenye akaunti nono ya maneno, Jose Mourinho amedaiwa kutaka kujiunga na Manchester United na kuichukua nafasi ya Louis Van Gaal.

Vyanzo vya karibu vya meneja huyo mtata kutoka Ureno vimeieleza ESPN FC kuhusu mpango wake wa kuhamia Old Trafford.

Imeelezwa kuwa wawakilishi wake tayari wameanza kufanya hatua za awali ili kukamilisha mkakati huo wa kukikalia kiti cha Van Gaal.

Mourinho anadaiwa kuwa na ndoto za muda mrefu za kuitumikia Manchester United na huenda kufukuzwa kwake na Chelsea alhamisi wiki hii kumemfungulia rasmi mlango hususan kutokana na kuboronga kwa timu hiyo chini ya Van Gaal.

Ikumbukwe kuwa Mwaka 2013, Mourinho alipigiwa chapuo ya kuwa mrithi wa Sir Alex Ferguson na mara kadhaa alikuwa akiisifia timu hiyo.

Duru zimeeleza kuwa Manchester United imetenga donge nono kwa ajili ya kumvuta Mourinho ambaye hujiamini na kujiita mtu maalum, ‘Special one’.

Kocha wa Manchester Louis Van Gaal alieleza kuwa ni jambo la ajabu duniani kumtimua kocha kwenye rekodi kubwa katika ulimwengu wa soka kama Mourinho.

Marekani Yainyima Tanzania Mabilioni kutokana na Kufutwa Matokeo Ya Zanzibar, Ukamataji Makosa ya Mtandao
Ben Pol afunguka kuhusu Tweet yake iliyomvaa Ali Kiba