Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli amewahakikishia wananchi wa Nanyamba, Tandahimba, na Newala Mkoani Mtwara kuwa Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya uhakika ili kuunganisha Kanda ya Kusini Kiuchumi na wananchi wa Mkoa huo kuendelea kufanya kazi kwa juhudi ili kuweza kujiletea maendeleo yao.
Ameyasema hayo katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo, ambapo amesema kuwa Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Mtwara-Tandahimba-Nanyamba yenye urefu wa kilometa 50 itakayogharimu kiasi cha Tsh. bilioni 86 na kumwagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe kutangaza zabuni ya ujenzi wa kilometa zingine na kufikia kilometa 100.
”Barabara hii itakuwa ni kiunganishi cha uchumi mikoa ya kusini, hatuwezi kushindwa kujenga kilometa 100, lengo letu kuu ni kuiunganisha Bandari yetu ya Mtwara na mizigo inayotoa Malawi,” amesema JPM
Aidha, amesema kuwa katika kuwainua wakulima wa Mkoa wa Mtwara, Serikali imetekeleza ununuzi wa korosho kutoka kwa wananchi wenye korosho zaidi ya kilo 1500, na Tsh Bilioni 50 tayari zimetengwa kwa ajili ya kuwalipa wakulima hao, na kwa upande wa wakulima wa korosho wenye kilo chini ya 1500 wamelipwa kiasi cha Tsh Bilioni 578.
Rais Magufuli amewahiza wafanyabiashara walanguzi wa zao la korosho ‘Kangomba’ kuacha kuwadhulumu wakulima wadogo kwa kuwapa bei ambayo hairidhishi huku wakijua wametumia gharama kubwa katika kuendeleza zao hilo, na kusema serikali ya Awamu ya tano haitarudi nyuma kuwatetea wakulima hao.
Hata hivyo, ameongeza kuwa miradi mingine inayotekelezwa serikali ya Awamu ya Tano kuwa ni pamoja na upanuzi wa bandari ya Mtwara, upanuzi wa uwanja wa Ndege na ukarabari wa mradi wa maji wa makonde ambao utagharimu kiasi cha Tsh. bilioni 160 zikiwa ni fedha za mikopo kutoka Serikali ya India unaowezesha ujenzi wa miradi ya maji katika miji 28 nchini.