Kocha mkuu wa kikosi cha Mwadui FC, Jamuhuri Kiwelu Julio, amekiri kusikitishwa na matokeo ya timu ya Simba dhidi ya Coastal Union katika mchezo hatua ya robo fainali ya michuano ya kombe la shirikisho, uliochezwa jana kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es salaam.

Julio ambaye aliwahi kukinoa kikosi cha Simba kwa nyakati tofauti, amesema imemuuma kama mdau wa soka nchini kuona kikosi cha Msimbazi kinashindwa kutimiza dhamira ya kuibuka na ushindi katika mchezo huo.

Amesema haamini kama Simba walicheza mchezo mbovu kiasi cha kuwapa nafasi Coastal union kuwafunga katika mchezo huo, ambao kila mmoja aliamini huenda timu hiyo kongwe nchini ingeibuka na ushindi wa mabao mengi zaidi kutokana na udhaifu wa kikosi cha Coastal Union ambao umeonekana siku za hivi karibuni.

Kocha huyo mwenye sifa ya kuwa na maneno mengi, amedai kwamba Simba walikua na kila sababu ya kufanya vyema kupitia michuano ya kombe la shirikisho ili kurejesha hadhi yao ya kushiriki kwenye michuano ya kimataifa, lakini kupotea kwa bahati hiyo kunamaanisha nguvu zao zinapaswa kuelekezwa kwenye michezo ya ligi kuu ambapo ni kugumu zaidi.

“Kwa upande wangu nasitika Simba kupoteza kupoteza mchezo wao wa robo fainali dhidi ya Coastal Union kwa sababu ilikuwa ni nafasi pekee kwao kuwakilisha taifa kwenye michuano mikubwa ya Afrika, lakini kwa bahati mbaya wamepoteza bahati hiyo. Sasahivi wanatakiwa waelekeze nguvu kubwa kwenye ligi kuhakikisha wanapata uningwa”,

“Siyo kwamba nawaogopa Simba, lakini kwa siku za hivi karibuni walikuwa kwenye kiwango bora ambacho nilijua kama wangeingia nusu fainali mashindano yangekuwa magumu zaidi kwa maana kwamba wao wanauchu wa kupata nafasi kwenda kushiriki michuano ya kimataifa”.

Katika hatua nyingine Julio, ametamba kuchukua ubingwa wa michuano ya kombe la shirikisho kutokana na kuamini hakuna timu ambayo inaamtisha katika hatua iliyosalia.

Amesema Simba ilikuwa inampa wakati mgumu kufuatia kiwango chao kizuri walichokionyesha katika baadhi ya michezo ya ligi kuu, lakini kuondolewa kwao kumempa ahuweni ya kuamini ni nafasi nzuri kwake kuendelea kutengeneza historia kwenye soka la bongo kupitia michuano ya kombe la shirikisho.

“Kutoka kwa Simba kwenye mashindano sasa mimi najiona nina-nafasi kubwa na watu wakumbuke FA imefia mikononi mwangu kupitia Tanzania Stars, miaka miwili tumewakilisha nchi kwenye kombe la washindi barani Afrika kupitia FA”.

Mwadui FC ni moja ya klabu ambazo zimesalia kwenye michuano ya kombe la shirikisho na leo usiku itapangwa katika ratiba ya nusu fainali ambayo itaonyeshwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha Azam Two ambacho kinamilikiwa na Azam Media.

Timu nyingine zilizofanikia kuingia katika hatua ya nusu fainali ya kombe la shirikisho ni Azam FC, Young Africans pamoja na Coastal Union.

Kapombe Kuishuhudia Azam FC Kwa Miezi Miwili Hadi Mitatu
CUF: Serikali Ya imemuadhibu Maalim Seif