Mwenyekiti wa Kampuni ya Ujenzi ya CRCC ya China, Fengchao Meng ameahidi kuwekeza kwa kushirikiana na Serikali katika kuboresha miundombinu ya mkoa wa Dodoma.

Hayo yamesemwa mapema leo Oktoba 10, 2016 wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokutana na Mwenyekiti huyo aliyeongozana na Mwenyekiti wa Kampuni nyingine ya Ujenzi ya CCECC ya China, Yuan Li pamoja na Katibu Mkuu wa Chama cha Urafiki kati ya Serikali za Tanzania na China, Joseph Kahama, walikutana ofisini kwa Waziri Mkuu Magogoni jijini Dar es salaam.

Majaliwa amesema kipaumbele cha Serikali kwa sasa ni uendelezaji wa Makao Makuu Dodoma.

Amesema kuwa China na Tanzania ni marafiki wa muda mrefu na mataifa hayo yanashirikiana vizuri katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali hivyo Serikali inatarajia mengi kutoka kwenye kampuni hiyo kupitia kwa mwenyekiti wake, Meng.

Majaliwa amesema Dodoma kuna fursa za uwekezaji kwenye sekta nyingi kama miundombinu, kilimo na viwanda. Hivyo wanaweza kuwekeza kwenye ujenzi wa nyumba za makazi, ofisi, huduma za kijamii na viwanda.

Kwa upande wake, Meng amesema kampuni yake itaungana na Serikali katika kuboresha Makao  Makuu ya Serikali na inatarajia kutuma wataalam wake mkoani Dodoma kuangalia maeneo ya uwekezaji.

Amesema kuwa wataraji kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu, nyumba za makazi, ofisi, maeneo ya kutolea huduma za jamii na teknolojia zitakazowezesha upatikanaji wa maji safi na salama.

Young Africans Kucheza Shamba La Bibi
Mwasapili: ‘Tulieni’ Pointi Tatu Ni Zetu