Katibu Mkuu mpya wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Dk. Vicent Mashinji amewataka wananchi kumpima kwa kazi yake baada ya muda mfupi na aliyekua Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Wilbroad Slaa.

Akiongea na waandishi wa habari hivi karibuni, Dk. Mashinji alisema kuwa ameweka mikakati mipya ya kuisuka Chadema kuanzia ngazi ya vijiji na kwamba kazi atakayoifanya itawapa nafasi Watanzania kumpima kama viatu vya Dk. Slaa vimemtosha au vimempwaya.

Dk. Mashinji amesema kuwa moja kati ya mikakati wanayokuja nayo ni kupunguza uanaharakati na kujiandaa kuongoza Serikali. Ameongeza kuwa kupitia mikakati yao mipya, wanataka Halmashauri zote zinazoongozwa na Chama Chao ziwe mfano wa kuigwa na kuwapa matumaini watanzania kuwa wanaweza kuongoza na kuleta maendeleo ya hali ya juu nchini.

Katika hatua nyingine, Dk. Mashinji akanusha kuwepo kwa upendeleo katika nafasi za Wabunge wa Viti Maalum. Alifafanua kuwa nafasi zilitolewa kwa kila mkoa na kwamba walipanga majina yote kwa kutumia vigezo stahiki.

“Hakuna upendeleo… na kwenye Baraza Kuu wote waliokuwa wanalalamika walikuwa wanajua, japokuwa kuna shinikizo la nje ya chama linaloingia ndani kuja kutuvuruga,” alisema.

Alisema kuwa chama hicho hakitaacha kamwe sera yake ya kupinga ufisadi.

Aveva Atangaza Kamati Ya Maendeleo Ya Ujenzi Wa Uwanja Bunju
Vincent Kompany Kuwakosa Paris Saint-Germain Kesho