Jeshi la Lebanon limesema limegundua tani zaidi ya nne za madini ya kemikali ya Ammonia Nitrate karibu na lango la bandari ya Beirut, sehemu ambapo ulitokea mlipuko mkubwa mwezi uliopita.
Kwa mujibu wa tamko la jeshi lililoripotiwa na shirika la habari la serikali, NNA, wahandisi wa jeshi la Lebanon wanalishughulikia jambo hilo.Wakati huo huo wanaofanya juhudi za uokozi wamesema wamepata ishara ya kuwepo watu chini ya vifusi vya majengo yaliyoanguka, na hivyo kuleta matumaini huenda wapo watu walionusurika hata baada ya mwezi mmoja tangu kutokea mripuko mkubwa kwenye bandari ya mji wa Beirut.
Mlipuko huo uliotokea Agosti 4, na kuua watu zaidi ya 200 na majeruhi takriban 5000 ulisababishwa na mlundiko wa kemikali kama hizo zenye nguvu kubwa ya kulipuka.